Pompeo awasili Brussels kwa mkutano wa mawaziri wa NATO
27 Aprili 2018Waziri mpya wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani Mike Pompeo amewasili mjini Brussels kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Ziara ya Pompeo inakuja siku moja tu baada ya kuidhinishwa hapo jana kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.
Mike Pompeo,mkurugenzi mtendaji wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA katika utawala wa huo huo wa Rais Donald Trump, alifunga safari kwa ziara yake ya kwanza rasmi kama Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani, saa chache tu baada ya kuapishwa.
Akizungumza baada ya kuwasili katika eneo la mkutano mjini Brussels, Pompeo alisema kuna sababu nzuri ya yeye kuhudhuria mkutano huo. "Kazi inayofanyika hapa leo ina thamani kubwa. Malengo yake yana umuhimu mkubwa kwa Marekani. Rais Donald Trump alitaka nihudhurie na ninafurahi kuwa nimefaulu, na ninatarajia kuwa na ziara ya kufana leo."
Jens Stoltenberg wa NATO aliyemkaribisha Pompeo katika makao makuu ya jumuiya hiyo alimpongeza kwa kuidhinishwa kwake kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani huku akisema kuwa ujio wake ni ushahidi wa kutoshajuu ya umuhimu wa jumuiya hiyo na namna ambavyo Pompeo amejitolea kwa NATO.
Stoltenberg ameendelea kusema: "Ninatarajia kufanya kazi nawe kuendelea kuimarisha NATO katika mazingira yanayohitaji usalama zaidi na kwamba uzoefu wako wa muda mrefu unakufanya kuwa mtu bora zaidi kuwa mwanadiplomasia mkuu wa Marekani"
Yanayojadiliwa katika mawaziri hao wa NATO
Jumuiya ya NATO imesema mawaziri wake wa mambo ya nchi za nje wanakutana kujadiliana kuhusu mahusiano na Urusi, pamoja na ujumbe ujao wa mafunzo kwa ajili ya Iran. Kadhalika wataandaa maandalizi ya mkutano wa kilele unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai.
Heather Nauert ambaye ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, amesema kuwa Pompeo akimaliza ziara yake mjini Brussels, ataelekea Mashariki ya Kati, ambapo atakutana na viongozi wa Israel, Saudi Arabia na Jordan kujadili masuala ya kikanda pamoja na yanayohusu nchi hizo na Marekani.
Pompeo amechukua nafasi ya Rex Tillerson ambaye alifutwa kazi na Rais Trump mwezi uliopita.
Pompeo alipata ushindi mdogo kupitia kamati ya mambo ya nje ya baraza la seneti. Alipata kura 57 huku maseneta 42 wakiupinga uteuzi wake. Pompeo ndiye mtu aliyepata uungaji mkono mdogo kabisa tangu utawala wa Jimmy Carter.
Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman