1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo yuko tayari kuzungumza na Iran

26 Julai 2019

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema yuko tayari kwenda Iran kufanya mazungumzo wakati ambapo kuna mvutano kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/3Mn50
USA |  Amerikanischer Außenminister Mike Pompeo in New York
Picha: Reuters/File Photo/D. Ornitz

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema yuko tayari kwenda Iran kufanya mazungumzo wakati ambapo kuna mvutano kati ya nchi hizo mbili, lakini pia ameyatolea wito mataifa mengine kuungana katika kikosi cha kulinda meli za mafuta zinazopita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.

Akizungumza kwenye mahojiano na televisheni ya Bloomberg, Pompeo amesema ataukubali wito wa kuzungumza moja kwa moja na watu wa Iran, iwapo atapata fursa ya kufanya hivyo. Amesema angependa kuzungumza na wananchi wa Iran na sio kufanya propaganda.

Pompeo ameyatoa matamshi hayo jana mjini Washington wakati ambapo Iran na Marekani ziko katika mvutano mkali kuhusu usafirishaji wa meli za mafuta kwenye Mlango Bahari wa Hormuz na hatua ya Iran kuidunguwa ndege isiyo na rubani ya Marekani.

Atetea vikwazo

Mwanadiplomasia huyo amevitetea vikwazo vipya vilivyowekwa dhidi ya Iran hivi karibuni kama sehemu ya kampeni ya Marekani kuongeza shinikizo kubwa kwa lengo la kuishawishi Iran ibadilishe sera yake ya kigeni kupitia kitisho cha kiuchumi.

Mvutano kati ya Iran na Marekani uliongezeka tangu mwaka uliopita baada ya Marekani kujiondoa katika mpango wa kimataifa wa nyuklia ikisema kuwa ni dhaifu na kuweka vikwazo vipya.

Iranisches Patrouillenboot vor Öltanker in Straße von Hormus
Wanajeshi wa Iran wakipiga doria kwenye Mlango Bahari wa HormuzPicha: AFP/A.Kenare

Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa Iran walitangaza hadharani uwezekano wa kufanyika mazungumzo, lakini matarajio ya mazungumzo hayo yaliyeyuka baada ya siku ya Jumatano kiongozi wa kidini, Ayatollah Ali Khamenei kusema kuwa Iran haitojadiliana na Marekani kwa namna yoyote ile.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umezidi kuingia dosari katika miezi mitatu iliyopita kutokana na mashambulizi dhidi ya meli ya mafuta katika Mlango Bahari wa Hormuz kwenye pwani ya Iran.

Katika mahojiano tofauti na kituo cha televisheni cha Marekani, Fox News, Pompeo amesema kwamba nchi hiyo tayari imeziomba Japan, Ufaransa, Ujerumani, Korea Kusini, Australia na mataifa mengine kujiunga na mpango wa usalama kwenye eneo la bahari katika Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa Pompeo, kila nchi ambayo ina nia ya kuhakikisha njia za baharini ziko wazi na mafuta ghafi na bidhaa nyingine zinaweza kusafirishwa kupitia Ujia wa Bahari wa Hormuz, zinahitaji kujiunga na mpango huo wa usalama.

Matamshi ya Pompeo yametolewa baada ya Iran siku ya Jumatano kufanya jaribio ya kile kinachoonekana kuwa kombora la nyuklia la masafa ya kati ambalo lilisafiri umbali wa kilomita 1,000. Afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, amesema hata hivyo kombora hilo halikuwa tishio kwa shughuli za usafirishaji baharini au wafanyakazi wowote wa Marekani katika eneo hilo.