Punda hatarini kutoweka Kenya
4 Machi 2020Mji wa Kitengela ni sehemu muhimu kwenye barabara inayoelekea nchi jirani ya Tanzania kupitia mpaka wa Namanga unaoyagawa maeneo ya kaunti ya Kajiado na wilaya ya Longido nchini Tanzania. Jamii za eneo hilo ni za wafugaji na punda ni mnyama muhimu kwenye maisha yao ya kila siku. Hata hivyo takwimu rasmi zinaashiria kuwa huenda punda akaadimika kwa sababu kasi ya kuwachinja na ile ya kuzaliana hazishabihiani.
Takwimu za sensa ya mwaka 2009 zinaikadiria idadi ya punda nchini Kenya kuwa milioni 1.8 ila hali halisi ni tofauti. Josephat Ngonyo ni mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za wanyama ,ANAW na anabainisha kwamba,''iwapo biashara ya punda itaendelea basi wataadimika ifikapo mwaka 2023. Shughuli ya kutengeza dawa ya kiasili ya Kichina iitwayo ejiao zinaiongeza kasi ya punda kuchinjwa na hilo litawafanya waangamie kwa sababu soko lipo,” alieleza.
Machinjio 4 yapo Kenya
Kwa sasa Kenya ina machinjio 4 rasmi ya punda ambayo ni Goldox iliyoko kaunti ya Baringo, Star Brilliant ya mjini Naivasha, Zilzha iliyoko Turkana na Fuhai ya kaunti ya Machakos. Uwepo wa viwanda hivyo unaaminika kuchangia katika wizi wa punda hata kutokea nchi jirani za Ethiopia na Tanzania. Wizi huo unazitatiza familia zinazowategemea punda kwa usafiri, kuteka maji na pato la kila siku.
Simon Sokoine ni mfugaji wa punda anayetokea eneo la Rombo nchini Tanzania na alielezea kuwa, "Hao wanaofanya hii shughuli ,sio kwamba ni watu ambao ukiwashika wana kitu cha kuwalipa.Wanasema ndio utapewa kondoo ama mbuzi maana kwa Wamasai huwezi kumtoza mtu faini sawa na Yule aliyeiba ng'ombe. Punda bado kwa wamasai ni akitu ambacho kiko chini sana.Ingekuwa ni ng'ombe ipo faini maalum. Kwa punda faini yake ni kitu hivihivi.Ndio maana wanajua sasa hivi nikishikwa hawanipeleki mahali." anafafanua.
Punda analiwa Kenya
Kwa mujibu wa sheria ya bidhaa za nyama ya mwaka 1999, punda yupo kwenye orodha ya wanyama wanaoliwa jambo linalowapa nguvu wamiliki wa machinjio kuendelea na kuipigania biashara hiyo. Judy Muriithi ni wakili kwenye shirika la kutetea haki za wanyama la ANAW nchini Kenya na anaweka bayana kuwa,”Kenya kwa sasa haina sharia yoyote maalum inayomuangazia punda kama mnyama.Sheria zilizopo zinawajumuisha wanyama wote kwenye kundi moja.”
Wizi unafanyika mipakani
Kulingana na takwimu, wizi mkubwa zaidi wa punda unaripotiwa kutokea kwenye kaunti za Turkana na Kajiado zinazopakana na Ethiopia na Tanzania.
Nchi jirani ya Tanzania imepiga hatua na kufanikiwa kuyafunga baadhi ya machinjio ili kuisitisha biashara ya kuuza punda. Albert Samson Mbwembo ni afisa wa maendeleo na mawasiliano katika shirika la kutetea maslahi ya wanyama mjini Arusha, ASPA na alisisitiza, "Kwa Tanzania vipo viwanda viwili vinavyochinja punda ila kwa sasa kiwanda cha Dodoma kilichoko katikati ya nchi kimefungwa. Kinachoendelea na uchinjaji ni kile kiwanda cha Shinyanga. Lakini kwa bahati nzuri serikali imeweka idadi maalum ya punda wanaochinjwa kwa siku, kwamba isipite 40 katika kile kiwanda,” alishikilia.
Kufikia sasa ni mataifa 18 barani Afrika yaliyopiga marufuku biashara ya punda. Bei ya punda mmoja kwa sasa imeongezeka kutokea dola 5 hadi 150 . Ngozi ya punda inauzwa kwa shilingi kati ya dola 150 na 180 jambo linalowapa mwanya wezi wa punda kuwachuna ngozi hata wakiwa hai. TM,DW Kitengela.