Putin asema maslahi ya Urusi hayana mjadala
23 Februari 2022Katika ujumbe wa vidio wakati wa maadhimisho ya siku ya watetezi wa taifa, ambayo ni siku ya mapumziko nchini humo, Putin amelipongeza jeshi la Urusi na kusifu utayarifu wa jeshi hilo kuingia vitani, baada ya kuashiria mipango ya kupeleka wanajeshi ndani ya Ukraine.
"Nchi yetu mara zote iko tayari kwa mazungumzo ya kweli na ya wazi, kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa matatizo magumu zaidi," Putin alisema.
Soma pia: Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine
Lakini akaongeza: "Maslahi ya Urusi, na usalama wa raia wetu ni mambo yasio na mjadala kwetu. Kwa hiyo tutaendelea kuimarisha na kuendeleza jeshi letu na jeshi la wanamaji, kuongeza ufanisi wao, na kuwapa vifaa vya kisasa zaidi."
Putin alizungumza baada ya baraza la juu la bunge la Urusi, jana jioni kumpa idhini kwa sauti moja, kupeleka vikosi vya kulinda amani kwenye mikoa mwili iliyojitenga nchini Ukraine, ambayo hivi sasa inatambuliwa na Moscow kama huru, na yumkini katika maeneo mengine ya Ukraine.
Jumanne usiku Urusi ilisema imeanzisha uhusiano wa kidiplomasia kwa ngazi ya ubalozi na mikoa hiyo iliyotangaza kujitenga na Ukraine mwaka 2014, katika mzozo uliosababisha vifo vya watu 14,000 mpaka sasa.
Soma pia: Viongozi wa dunia wailaani Urusi kuhusu Ukraine
Akizungumza na waandishi habari jana jioni, Putin aliorodhesha masharti makali ikiwa mataifa ya magharibi yanataka kutuliza mzozo huo, akisema Ukraine, ambayo inaelemea upande wa magharibi inapaswa kuachana na mipango yake ya kujiunga na NATO, na kubaki bila upande.
Marekani, washirika watangaza vikwazo vikali
Rais wa Marekani Joe Biden, siku ya Jumanne alitangaza vikwazo vipya vikali dhidi ya Urusi, lakini alisema bado kuna muda wa kuepusha vita. Japana na Australia zilifuata mara moja mapema leo kwa kutangaza vikwazo vyao vikali kwa Moscow na watu wanaohusishwa na uhasama dhidi ya Ukraine.
Ujerumani pia ilitangaza kusitisha mchakato ya kuidhinisha mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Urusi kwenda nchini humo, linalojulikana kama Nord Stream 2. Lakini Urusi imejigamba na kusema vikwazo hivyo vitaenda upogo.
Soma pia: Urusi yakabiliwa na vikwazo
Mipango ya Putin imesalia kuwa kitendawili, lakini maafisa wa magharibi wamekuwa wakionya kwa wiki kadhaa kwamba amekuwa akijiandaa kwa ajili ya uvamizi kamili wa Ukraine, hatua ambayo inaweza kusababisha vita mbaya barani Ulaya.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, amsema muungano huo wa kijeshi una kila ishara kwamba Moscow inaendelea kupanga shambulio kamili dhidi ya Ukraine.
Chanzo: Mashirika
Mhariri: Josephat Charo