1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Burundi wakwama katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

30 Machi 2020

Raia kadhaa wa Burundi wamekwama katika mpaka kati ya Tanzania na Burundi baada ya serikali ya Burundi kufunga mpaka wake katika eneo la Manyovu mkoani Kigoma kufuatia kuwepo kwa tishio la Virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3aBRB
Archivbild - Burundi's President Pierre Nkurunziza
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Raia kadhaa wa Burundi wamekwama katika eneo la mpaka kati ya Burundi na Tanzania baada ya zuio la kuwataka wasafiri kutoka Tanzania kutoingia Burundi. Akiongea na waandishi wa habari kwa niaba ya wenzak, Damas Achimani anadai wao ni raia wa Burundi na wanazo hati za kusafiria na walikuwa wakirejea nyumbani kabla ya kukutwa na kuzuizi hicho.

Damani anasisitiza kuitaka Burundi kuanzisha kituo cha upimaji na matazamio ya virusi vya Corona.

Mwishoni mwa juma Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dr. Damas Ndumbalo alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bi. Jelly Maleko katika eneo la Manyovu mpakani ambapo walikubaliana kuongeza udhibiti wa mwingiliano wa watu katika mpaka wa nchi hizo ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Wakati huo huo wakimbizi wa Burundi na DRC waishio nchini Tanzania wameelezea kuishi kwa hofu ndani ya kambi kwa sababu ya COVID19 na kueleza kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu maambukizi ya virusi hivyo, Wakiongea na DW wakimbizi walioko katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma wamekiri kuona jitihada za serikali na shirika la UNHCR lakini elimu haijasambaa.

Taarifa zinaeleza kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa na mashirika yanayohudumia wakimbizi katika kukabiliana na Corona ni kuongeza idadi ya mgao wa sabuni na kuimarisha huduma za maji makambini