Raia wa Burundi wanalalamikia muda mfupi wa kubadili pesa
12 Juni 2023Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wiki chache zilizopita aliwatahadharisha walioweka fedha nyingi majumbani kwamba ipo siku watakapozikuta hazina thamani.
Madalali wa mabasi wakataa noti za zamani
Katika maeneo tofauti ya umma, shughuli za kununuwa na kuuza bidhaa ama huduma zimetatizika. Kwenye usafiri wa mabasi madalali wamekuwa wakikataa noti za zamani za elfu 5 na zile za elfu 10 na kuwataka abiria kulipa kwa kutumia noti mpya ambazo bado hata hivyo kupatikana kwa kiwango cha kutosha.
Wafanya biashara wawalazimisha wateja kutumia noti mpya
Hali kama hiyo inashuhudiwa pia kwenye masoko na hata madukani, ambapo wafanya biashara wanawalazimisha wateja kulipa kwa noti mpya, wakati muda uliotolewa na benki kuu ya Jamhuri hadi Juni 18 bado haujafikia mwisho.
kuna idadi ndogo ya pesa katika mzunguko wa fedha nchini
Akitangaza hatua hiyo ya kubadili ghafla fedha hizo, naibu mkuu wa Benki Kuu ya Jamuhuri Desire Musharitse alisema kumekuwa na idadi ndogo ya pesa katika mzunguko wa fedha nchini. Huku noti za elf 10 na zile za elf 5 zikionekana kuadimika na hivyo kutatiza shughuli za benki na mashirika ya kifedha kukwama.
Hatua hiyo inaonekana kuwa na muingilio wa kisiasa
Juvenal Bigirimana mwandishi habari anasema hatua hiyo inaonekana kuwa na siasa ndani yake, kwani wanaoshukiwa kuhusika na wizi wa mali ya umma wanatajwa kuficha mabilioni ya pesa majumbani.