Raia wa India kizani kwa muda wa siku mbili mfululizo
31 Julai 2012Kupotea kwa umeme nchini India kumeathiri majimbo19 katika maeneo ya Kaskazini, Mashariki, kaskazini mashariki na hata mji mkuu wa nchi hiyo New Delhi. Kulingana na maafisa nchini humo nyaya za kupitisha umeme ziliharibika usiku wa saa saba na dakika kumi kwa saa za India baada ya kisa kama hicho kutokea tena hapo jana na kukatiza huduma za usafiri pamoja na maji.
Baada ya muda kidogo nazo nyaya za mashariki mwa India pia zikakumbwa na matatizo kama hayo kisha ikafuata zamu ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kwa pamoja nyaya hizo zinatoa umeme katika maeneo ambayo yanakaliwa na karibu nusu ya idadi ya watu nchini India ya bilioni 1.2, kwa hiyo kwa ujumla wale walioathirika na matatizo hayo ya kukosea umeme haswaa katika maeneo ya mashinani ni zaidi ya watu milioni 300.
Inaripotiwa kwamba nyaya hizo za kuzalisha umeme zilikwama kufanya kazi kutokana na mahitaji makubwa ya umeme katika majira haya ya joto kali la kiangazi.
Hata hivyo maelfu ya watu walikwama katika vituo vya usafiri wa treni, baada ya hali hiyo kuathiri zaidi ya treni 300 kaskazini mwa nchi. Kando na hilo biashara, huduma katika hospitali, na huduma nyengine muhimu zilikuwa zinatolewa kwa kutumia umeme mbadala. Wakaazi sasa wanalalamika kuwa hakuna mtu wa kuwapa majibu kamili ya kwanini jambo kama hili linatokea.
kukatika kwa umeme mara kwa mara sio jambo geni nchini India, na Itakumbukwa kuwa ni mwaka huu tu ambapo kulikuwa na maandamano makubwa kufuatia kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini humo. Lakini hatua hii ya kuharibika kwa nyaya za kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa hakijawahi kushuhudiwa nchini India.
Mara ya mwisho kwa tukio kama hili kutokea ni katika eneo moja tu la kaskazini ambapo nyaya zake ziliharibika mwaka wa 2001. Hata hivyo kwa sasa umeme unaripotiwa kuanza kuonekana katika maeno kadhaa japo kwa uchache.
Huku hayo yakiarifiwa hii leo India imefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri ambapo waziri wa nishati Sushilkumar Shinde amehamishwa hadi katika wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo wakati ambapo India inakabiliwa na tatizo kubwa la Umeme.
P. Chidambaram Waziri wa mambo ya ndani naye kwa sasa ndiye waziri mpya wa fedha nchini India. Hii ni kulingana na afisaa mmoja mkuu katika ofisi ya rais Sharat Chandra aliyezungumza na chombo cha habari cha AFP.
Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP
Mhariri Mohammed Abdul-Rahman