Raia Kongo wafurahia kuondoka wanajeshi wa Afrika Mashariki
4 Desemba 2023Raia kadhaa waliozungumza na mwandishi wa DW mkoani Kivu Kaskazini siku ya Jumatatu (Disemba 4) walisema kuwa hatua hiyo ingelilipa "nguvu jeshi la serikali ya Kongo kulitokomeza kundi la waasi wa M23", ambalo limekuwa likifanya mashambulizi na kushikilia maeneo kadhaa mashariki mwa nchi hiyo.
Kundi hilo la kwanza la wanajeshi 100 wa Kenya liliondoka Kivu Kaskazini kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Goma siku ya Jumapili (3 Disemba).
Soma zaidi: Waasi wa M23 waudhibiti mji wa kimkakati wa Kitshanga
Askari hao waliokuwa wakishutumiwa na mashirika ya kiraia kushirikiana na kundi la waasi wa M23 wameondoka wakati hali ya usalama ikiendelea kuwa tete katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.
Kabla ya wanajeshi hao kuondoka, kamanda wa Kikosi cha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Francis Ogolla, aliwapongeza kwa kile alichosema "wamepata mafanikio makubwa" tangu kupelekwa kwao katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
M23 kuchukuwa maeneo yaliyoachwa na Kikosi cha Afrika Mashariki
Wakati huo huo, kundi la M23 lilitangaza kuwa lingelichukuwa maeneo yote yaliyokuwa chini ya uongozi wa kikosi hicho cha kikanda.
Mmoja wa wasemaji wa kundi hilo, Willy Ngoma, alithibitisha kuwa huo ndio mpango wa waasi hao, ambao ungelianza kutekelezwa mara moja.
Kufikia asubuhi ya siku ya Jumatatu (Disemba 4), mwandishi wa DW mashariki mwa Kongo aliripoti kuendelea kusikia milio ya silaha nzito kwenye mji mdogo wa Malehe ulio umbali wa kilomita nane kutoka Sake.
Soma zaidi: Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke DRC
Kulingana na mratibu wa asasi za kiraia wa wilaya ya Masisi, Telesphore Mitondeke, milio hiyo yalikuwa ni mashambulizi ya waasi wa M23 "waliokuwa wanazilenga kwa makombora ngome za jeshi la Kongo."
Hofu ilikuwa imetanda katika mji wa Mushaki ambako mamia ya raia wameanza kukimbia nyumba zao kuelekea tena mji wa Sake ulio umbali wa kilomita 27 kutoka Goma.
Imetayarishwa na Benjamin Kasembe/DW Goma