1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Namibia washiriki uchaguzi wa Rais

Angela Mdungu
27 Novemba 2024

Wananchi wa Namibia wameshiriki katika zoezi la kupiga kura Jumatano ili kumchagua Rais wa taifa hilo. Ni uchaguzi unaotajwa kuwa huenda ukawa mtihani mkubwa kwa chama tawala cha SWAPO kurejea madarakani.

https://p.dw.com/p/4nUlZ
Uchaguzi Mkuu Namibia
Mgombea Urais na Makamu wa Rais wa Namibia kupitia chama tawala cha SWAPO, Netumbo Nandi-Ndaitwah Picha: Noah Tjijenda/REUTERS

Miongoni mwa waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa leo katika mji mkuu Windhoek ni makamu wa Rais na mgombea wa chama tawala cha SWAPO Netumbo Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72. Kama ataibuka mshindi, Nandi-Ndaitwah atakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini humo.

Chama chake kimelitawala taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa miaka 34 tangu kilipoliongoza kupata uhuru mwaka 1990.   Mpinzani mkubwa wa makamu huyo wa rais katika uchaguzi huu ni Panduleni Itula wa chama cha upinzani cha Independent Patriots for Change IPC. Mwaka 2019 Itula mwenye miaka 62 alipata asilimia 29 ya kura kama mgombea huru.

Soma zaidi: Namibia yapiga kura huku chama tawala kikikabiliwa na kinyang'anyiro kikali

Mgombea huyo amesema ana imani chama chake kitafanya vizuri kwenye uchaguzi huo. Kwa mujibu wa tume ya  uchaguzi ya Namibia, karibu watu milioni 1.4 wameandikishwa kupiga kura katika taifa hilo lenye watu milioni tatu.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2019 uungwaji mkono wa chama tawala cha SWAPO ulishuka kwa asilimia 56 kutoka asilimia 87 za mwaka 2014.  Ili kuchaguliwa kuwa Rais, mgombea anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura, vinginevyo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi.

Uchaguzi wa Namibia
Rais wa Namibia Nangolo Mbumba akipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Namibia, Novemba 27.11.2024 Picha: Noah Tjijenda/REUTERS

Rais wa mpito anayetetea kiti chake hagombei Urais

Kwa sasa, Namibia inaongozwa na rais wa mpito Nangolo Mbumba aliyeingia madarakani mwezi Novemba baada ya kifo cha Rais wa zamani Hage Geingob. Mbumba hagombei katika uchaguzi huu. Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa baada ya siku mbili.

Taifa la Namibia limekuwa ikishuhudia kukua kwa uchumi katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uwekezaji katika mafuta, gesi ya hydrogen ya kijani. Licha ya hilo, nchi hiyo inashika nafasi ya pili kwa ukosefu wa usawa katika kipato, kwa mujibu wa takwimu za benki ya dunia.

Wataalamu wanabashiri chama tawala cha SWAPO kupata wingi wa kura za bunge licha ya kukabiliwa na ukosoaji kutokana na uchumi dhaifu, uhaba wa wawekezaji katika sekta ya afya pamoja na tatizo la rushwa.