Raia wa Sierra Leone wanapiga kura leo
24 Juni 2023Katika uchaguzi huo rais wa sasa Julius Maada Bio wa chama cha Sierra Leone People's Party (SLPP) anawania kutetea kiti chake. Mshindani mkuu wa Bio ni Samura Kamara wa chama cha All People's Congress (APC).Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu saa moja asubuhi na zoezi litaendelea hadi saa kumi na moja jioni.
Soma zaidi: Sierra Leone yapiga marufuku mikutano ya kisiasa mitaani
Wagombea urais ni lazima wapate asilimia 55 ya kura au zaidi ili kutangazwa mshindi kwenye duru ya kwanza. Kulingana na msemaji wa tume ya uchaguzi, takriban watu milioni 3.4 wamejiandikisha kupiga kura, asilimia 52.4 kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 35.
Kupanda kwa bei ya vyakula ni suala muhimu kwa wapiga kura wengi katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Wapiga kura pia watawachagua wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa katika mfumo uliofanyiwa mabadiliko za dakika ya mwisho. Shirika la fedha la kimataifa, IMF na wanahabari wasio na mipaka wametoa wito kwa mamlaka kulinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi.