Rais Biden asema NATO ndio muungano imara zaidi
22 Februari 2023Rais Joe Biden na mwenzake wa Poland Andrzej Duda wamefanya mazungumzo yao katika ikulu ya rais mjini Warsaw saa chache kabla ya hotuba inayosubiriwa ya kiongozi huyo wa Marekani kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine. Kwenye mazungumzo yake na rais Duda,rais huyo wa Marekani amesema nchi yake inaendelea kuiunga mkono Ukraine kwa dhati lakini pia ametanabahisha kwamba jumuiya ya kujihami ya NATO ni imara kuliko ilivyowahi kuonekana.
"Tunapaswa kuwa na usalama barani Ulaya,ni jambo la msingi na muhimu. Kwahivyo Jumuiya ya NATO ni muungano muhimu na naweza kusema ndio muungano muhimu zaidi katika historia na sio tu katika historia mamboleo lakini katika historia kwa ujumla. Na kwahivyo nimeweka wazi kwamba msimamo wa Marekani na washirika wake ni thabiti na mwaka mmoja baada ya uvamizi wa Urusi naweza kusema kwamba NATO ni imara kuliko wakati mwingine''
Na kwenye hotuba atakayoitowa jioni hii Biden anatarajiwa kuzungumzia kuhusu kujitolea kwa Poland na washirika wengine wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO na wasiokuwa wanachama wa jumuiya hiyo katika eneo la Ulaya Mashariki katika kuiunga mkono Ukraine.
Hotuba ya Biden inakuja katika wakati ambapo rais wa Urusi Vladmir Putin amezikosoa nchi za Magharibi akisema ndio waliochochea vita hivyo vya Ukraine na kwamba nchi yake pamoja na jirani yake Ukraine wote ni wahanga wa undumilakuwili wa nchi za Magharibi. Putin amekwenda mbali kwa kusema wananchi wa Ukraine wamekuwa mateka wa serikali yao mjini Kiev na mataifa ya magharibi walioikalia nchi hiyo.
Rais huyo wa Urusi pia hakuonesha ishara yoyote ya kutaka kubadili mkakati wake katika vita vyake nchini Ukraine vilivyosababisha umwagaji mkubwa wa damu na badala yake ameuzidisha mvutano na nchi hizo za Magharibi kwa kujiondowa kwenye mkataba pekee uliobakia na Marekani wa kudhibiti uundaji wa silaha za Nyuklia unaofahamika kama START.
Hatua hiyo ya Urusi imekosolewa vikali na Jumuiya ya kijeshi NATO huku katibu mkuu wa mfungamano huo Jens Stoltenberg akisema uamuzi wa Urusi unaifanya dunia kuwa mahala hatari zaidi na kumtolea mwito Putin kutafakari tena msimamo wake. Urusi na Marekani zilisaini tena mkataba huo wa START mnamo mwaka 2010 nchi zote mbili zikiahidi kupunguza uundaji wa vichwa vya Nuklia na matumizi ya makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa hivyo vya Nyuklia.
Rais Vladmir Putin kwa upande mwingine pia ameitaka nchi yake kujiandaa kuanza tena majaribio ya silaha zake za Nyuklia ikiwa Marekani itachukuwa uwamuzi wa kufanya hivyo,hatua ambayo inaweza kuondowa marufuku iliyowekwa duniani ya kufanyika majaribio aina hiyo tangu kumalizika enzi ya vita baridi .