Tshisekedi asema simu za kiganjani zina damu ya Wakongo
30 Aprili 2024Nchi zilizoendelea kiviwanda ‘lazima ziweke shinikizo kwa [mashirika ya kimataifa] kukomesha biashara haramu. ... Simu za kiganjani mlizo nazo hapa katika nchi zenu zina damu ya Wakongo.’ Ndivyo alivyosema Félix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika mahojiano maalum na DW mjini Berlin.
Tshisekedi alisema '‘Rwanda imegundua kuwa kuna madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikajenga mitandao ya mawasiliano katika jumuiya ya kimataifa ambayo imeiwezesha kuwa muuzaji wa rasilimali hizi za damu zilizochukuliwa kwa nguvu na kuwalazimisha watu wetu kuondoka katika maeneo yao zinakopatikana raslimali hizo.''
Tangu wakati huo, aliongeza kusema Tshisekedi, ''Rwanda imekuwa wakala wa malighafi kimataifa na kwa mashirika ya kimataifa.''
Adai Rwanda inajitajirisha kwa rasilimali za Kongo
Rais huyo wa DRC ameendelea kueleza kuwa '‘Rwanda haina viwanda vinavyoweza kuifanya nchi hiyo kuwa tajiri sana,'' na kudai kuwa ''haya ni matokeo ya uporaji wa malighafi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.'’
Kuhusu makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Rwanda ya kuendeleza minyororo ya thamani ya malighafi, Tshisekedi alisema: ‘Hii ni kama bonasi kwa vita na uporaji. ... ni kashfa kwamba Umoja wa Ulaya unajivunia mkataba kama huo.’'
Aidha, Félix Tshisekedi amemkosoa Rais wa Rwanda Paul Kagame akisema ‘'kila kitu kinahujumiwa na Kagame na utawala wake.’'
Katika mahojiano hayo na DW, kiongozi huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema ana nia ya ‘kutoa fursa kwa ajili ya amani'', akisisitiza kuwa huo lakini ''si udhaifu na subira yetu haitadumu milele.’'
Akizidi kumzungumzia mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, alimtaja kuwa 'mchokozi na mhalifu.' ''Na ninataka kukutana naye ... nimwambie moja kwa moja tukitazama machoni kuwa yeye ni mhalifu na inatosha. Kila mtu amekwishaujua mchezo wake, na yale aliyoifanyia nchi yangu na watu wangu yanatosha, na kwamba huu ni wakati wa kuondoka kwenye ardhi ya nchi yangu.’
Kansela Olaf Scholz aalikwa kuizuru Kongo
Ama kuhusu uushirikiano wa kiuchumi baina ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ujerumani, Tshisekedi alisema ‘ninamwalika Kansela wa Shirikisho la Ujerumani kuitembelea Kongo. ... Tuna mahitaji mengi katika sekta ya miundombinu, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. ... Inahitaji nishati, na nishati safi hasa kwa wakati huu. Kongo ina utajiri hapa. Sasa tunahitaji uwekezaji ili kuendeleza haya yote.''
Alisema vipaumbele vya Kongo pia ni pamoja na elimu, afya, uwekezaji katika mfumo wa kidijitali na teknolojia mpya, ambazo zinapendwa sana na vijana wa nchi hiyo. ''Zaidi ya asilimia 60 ya watu wetu wana umri wa kati ya miaka 0 na 30,'' alisema Tshisekedi.