Rais Kenyatta atangaza ukame kuwa janga la kitaifa Kenya
9 Septemba 2021Ameagiza Wizara ya Fedha na Usalama wa Taifa kuongoza juhudi za serikali kuhakikisha kila familia iliyoathirika inapata mahitaji ya msingi.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Ikulu Kanze Dena Mararo amesema kuwa uamuzi huo, unafuatia mkutano kati ya Kiongozi wa taifa na viongozi 85 kutoka maeneo yenye ukame, wakiongozwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.
Wakenya milioni mbili tayari wanaathiriwa
Kwa mujibu wa serikali, takriban Wakenya milioni mbili kutoka majimbo 10 wanakabiliwa na ukame. Hawa ni baadhi ya wakazi wa jimbo la Wajir wanaokabiliwa na makali ya ukame huo.
soma pia: Wakenya milioni 1.4 wakabiliwa na njaa
Wametembea mwendo mrefu kutafuta maji na malisho ya mifugo. Wafugaji wa kutoka majimbo ya Isiolo na Garissa pia wamefika kwenye kisima hiki, hali inayosababisha mzozo, imeripotiwa kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita watu saba wamefariki kutokana na mizozo hiyo.
Taarifa hiyo ya Ikulu imesema, maelezo zaidi yatatolewa kwa umma, ya jinsi ya kuangazia tatizo hilo.
Mwezi uliopita ripoti ya Shirika la Msalaba Mwekundu ilielezea mpango wa dharura wa kukabiliana na hali ya ukame. Ukame huo umechangiwa na uhaba wa mvua katika miezi ya Oktoba-Desemba mwaka 2020 na mwezi Machi na Mei mwaka huu kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Mwezi Juni mwaka huu, maeneo mengi ya ukame, yalipata mvua ya wastani wa asilimia 50, iliyosababisha kupungua kwa mazao na mimea katika miezi iliyofuatia.
Asha Mohammed ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya, amesema ni lazima jamii zote ziungane pamoja kuangazia suala hilo.
"Tunajua kuwa kila mtu ana na shida wakati huu, kama sio shida ya chakula ni mahitaji mengine. Watoto wengi wengi wameathiriwa lazima tuone jinsi ya kuwasaidia,” amesema Mohammed.
Shirika la Msalaba Mwekundu linalenga kuzisaidia familia 100,000 katika kipindi cha miezi sita ijayo kwa ushirikiano na mashirika ya serikali katika ngazi za taifa na majimbo.
Majimbo katika maeneo kame yathiriwa zaidi
Majimbo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na Turkana, Garissa, Wajir na Marsabit, kwa mujibu wa Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Ukame. Mashirika ya kibinadamu yanasema kuwa, majimbo hayo hayajakuwa na mavuno ya kutosha na kwamba visima vyao, vimekauka.
Mvua zinazotarajiwa kunyesha mwezi Oktoba hadi Disemba huenda zikabainisha iwapo hali katika maeneo kame itaimarika.
Taifa la Kenya hukabiliwa na ukame wa mara kwa mara kwani ni asilimia 20 tu ya taifa hilo ambayo hupokea mvua za mara kwa mara.