Rais Kibaki kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika
31 Januari 2008Rais Mwai Kibaki wa Kenya anaondoka leo mjini Nairobi kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuondoka mjini humo mwendo wa saa moja unusu asubuhi ya leo licha ya mzozo wa kisiasa unaoendelea kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.
Atakapokuwa mjini Addis Ababa rais Kibaki atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa shirika la maendeleo la kanda ya Afrika Mashariki, IGAD.
Chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM, kilimtuma katibu mkuu wake, Profesa Anyang Nyong´o mjini Addis Ababa mapema juma hili kuushinikiza Umoja wa Afrika usimruhusu rais Kibaki kuhudhuria mkutano huo.
Chama hicho kinadai kumualika rais Kibaki katika mkutano wa mjini Addis Ababa ni kutambua rasmi kuchaguliwa kwake tena na kuzihujumu juhudi za upatanisho zinazoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan.
Mazungumzo kati ya pande zinazozana yanaingia siku yake ya pili hii leo huku shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu, Amnesty International, likiitolea mwito serikali ya Kenya iwalinde wanaharakati wa haki za binadamu, ambao baadhi yao wamepokea vitisho vya kuuwawa kwa kulaani udanganyifu uliotokea katika uchaguzi uliopita.
Maafisa tisa, wakiwemo wanaume sita na wanawake watatu wamepokea ujumbe unaowashutumu kwa kuyasaliti makabila yao.