Rais Lula alazwa baada ya damu kuvuja kwenye ubongo
10 Desemba 2024Hospitali ya Sirio Libanes katika mji mkuu Brasilia imesema leo kuwa rais huyo mwenye umri wa miaka 79 alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu jana jioni baada ya kupata maumivu ya kichwa. Uchunguzi baadaye uligundua kuvuja damu kwenye ubongo, kulikosababishwa na jeraha la kichwa alilolipata mnamo Oktoba 19.
Rais huyo alihamishiwa kitengo kingine cha hospitali hiyo mjini Sao Paulo, ambako alifanyiwa upasuaji wa kuondoa damu iliyoganda kwenye ubongo. Hospitali hiyo imesema upasuaji huo ulikwenda vizuri na rais anaendelea kupata nafuu katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Lula alifuta kuhudhuria mkutano wa kilele wa kundi la BRICS katika mji wa Urusi wa Kazan mwishoni mwa Oktoba kutokana na jeraha la kichwa. Rais huyo alijigonga kichwa baada ya kuanguka bafuni katika makazi ya rais mjini Brasilia.