Rais Mnangagwa ataka vikwazo dhidi ya Zimbabwe viondolewe
26 Septemba 2019Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameomba uvumilivu, huku akiongeza juhudi za kufufua uchumi wa nchi yake ulioporomoka.
Aidha Mnangagwa amezitolea wito Marekani na nchi za Ulaya kuondoa vikwazo alivyovitaja kuwa ni kinyume cha sheria ilivyowekewa nchi yake na ambavyo vinaizuia kuimarika kiuchumi.
Wakati akihutubia katika Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa hapo jana. Mnangagwa hakutaja madai ya ukandamizaji wa kisiasa unaoendelea chini ya utawala wake nchini Zimbabwe.
Zaidi ya wakosoaji wa serikali 50 pamoja na wanaharakati wamekamatwa nchini Zimbabwe mwaka huu, wakati wengine wakiteswa na kuonywa na maafisa wa usalama kuachana na harakati zao za kuikosoa serikali.
Wakosoaji wanamshutumu Mnangagwa kwa kutumia mbinu za ukandamizaji dhidi ya upinzani wa serikali unaozidi kupata nguvu huku kukiwa na mfumko wa bei, uhaba wa maji na mgao wa umeme.