1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mteule wa Malawi Lazarus Chakwera ni nani?

28 Juni 2020

Rais mteule wa Malawi Lazarus Chikwera ni mhubiri wa zamani injili ambaye anasema alijiunga na siasa ili kuitia wito wa Mungu.

https://p.dw.com/p/3eRgy
Lazarus Chakwera Präsidentschaftswahlen Kandidat Malawi
Rais Mteule wa Malawi, Larazus ChakweraPicha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

"Siku moja Mungu alizungumza na moyo wangu na Mungu hakusema ananiondoa kuwa mhubiri, Mungu alikuwa akisema ninatanua kanisa lako ili uwe mhubiri wa taifa zima" alisema Chakwera katika video ya hivi karibuni wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kwa miaka saba iliyopita Chakwera mwenye umri wa miaka 65 amekiongoza chama kikongwe zaidi cha siasa nchini Malawi Congress Party (MCP), ambacho kililiongoza taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa miongo mitatu tangu mwaka 1964 hadi mwaka 1994 chini ya utawala wa chama kimoja chini ya kiongozi wa kiimla Hastings Kamuzu Banda

Chakwera alikiongoza chama hicho wakati wa uchaguzi wa raia wa mwaka 2014 na kushika nafasi ya pili nyuma ya rais anayeondoka madarakani Peter Mutharika.

Kadhalika aliwania tena kiti cha urais mwaka uliopita na kushindwa lakini uchaguzi huo baadaye ulibatilishwa.

Chama cha MCP kimepoteza chaguzi tano za urais tangu mwaka 1994 lakini Chakwera alifanya kazi kubwa ya kurejesha tena haiba ya chama hicho kwa kujitenga na utawala wa mkono wa chuma wa Banda na kuimrisha tena ngome ya chama hicho.

Uchaguzi wa mwaka 2019 ulikuwa wa tofauti 

Malawi Lilongwe | Neuwahlen | Beamte überprüfen Wählerlisten
Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Baada ya kushindwa na Mutharika kwa ushindi mwembamba wakati wa uchaguzi wa mwaka uliopita, Chakwera alianzisha kile kilichokuja kufahamika kuwa mchakato wa kihistoria wa kisheria.

Uchaguzi huo ulibatilishwa na mahakama ya juu ya Malawi iliyobaini osari nyingi ikiwemo matumzii ya wino wa kufanyia masahihisho katika karatasi za matokeo.

Uamuzi huo ulilitikisa bara la Afrika ambako ni nadra kwa viongozi walio madarakani kushindwa uchaguzi au kesi katika mahakama za mataifa yao.

 Mahakama iliamuru kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na kulingana na tume ya uchaguzi Chakwera amepata ushindi wa zaidi ya asilimia 58 ya kura.

"Watu wanataka mabadiliko. Wanahitaji mabadiliko na wanatuona sisi kuwa taswira ya mabadiliko" amesema Chakwera alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Wakati wa uchaguzi wa marudio Chakwera alipata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa makamu wa rais Saulos Chilima, rais wa zamani Joyce Banda na vyama kadhaa vidogo.

Lazarus Chakwera ni nani ?

Malawi Opposition Lazarus Chakwera
Picha: Reuters/E, Chagara

Chakwera alizaliwa mjini Lilongwe na mkulima mdogo ambaye watoto wake wawili wa kwanza wa kiume walifariki wakiwa wachanga. Alipewa jina la Lazarus sawa na mtu mmoja aliyetajwa ndani ya biblia kuwa alifufuliwa kutoka wafu.

Alisomea falsafa na theolojia na kuwa rais wa madehebu ya wapentekoste kuanzia mwaka 1989 hadi 2013 alipochukua hatamu za uongozi wa chama cha MCP.

Kwa miaka mingi alikuwa mwanaharakati wa utawala bora katika kamati inayoheshimika nchini Malawi ya masuala ya umma (PAC) ambayo ni mkusanyiko wa asasi za kidini na kiraia.

Mara zote Chakwera alifungua mikutano yake ya kampeni kwa sala.

Chakwera anayezungumza kingereza cha lafudhi ya Marekani anasema anapenda kujisomea, kusikiliza muziki wa asili, miondoko ya country na nyimbo za injili.

Rais huyo mteule ameoa na ana watoto wanne.