1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni afanya mabadiliko ya watendaji wa serikali

22 Machi 2024

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemteua mwanawe wa kiume jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa mkuu wa jeshi la ulinzi nchini humo na kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri.

https://p.dw.com/p/4e0Uz
Uganda |  Muhoozi Kainerugaba
Jenerali Muhoozi KainerugabaPicha: Lubega Emmanuel/DW

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemteua mwanawe wa kiume jenerali Muhoozi Kainerugabakuwa mkuu wa jeshi la ulinzi nchini humo.

Taarifa ya jeshi la nchi hiyo imesema kuwa Kainerugaba aliteuliwa katika wadhifa huo jana jioni.  Washauri wake wawili wa karibu pia wameteuliwa katika nyadhifa za uwaziri katika mabadiliko ya baraza la mawaziri ambayo pia yalitangazwa jana jioni na kuibua uvumi kwamba Museveni anaunga mkono shughuli za kisiasa za Kainerugaba.

Uteuzi wa Kainerugaba ni hatua ya kutatanisha katika taifa hilo ambalo kwa muda mrefu, watu wengi wameamini kuwa Rais Museveni anamtayarisha mwanawe kurithi kiti cha urais.

Katika siku za hivi karibuni, Kainerugaba, amekuwa akifanya mikutano ya hadhara kote nchini humo kinyume na sheria inayowazuia maafisa wa jeshi kujihusisha na siasa zinazoegemea upande mmoja, lakini amejitetea kwa kusema kuwa shughuli zake ikiwa ni pamoja na uzundiuzi wa hivi karibuni wa kundi la uanaharakati linalojulikana kama Patriotic League of Uganda zinalenga kuhimiza uzalendo miongoni mwa raia wa Uganda.