1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Museveni ataka kikosi cha AMISOM kiimarishwe

Kabogo Grace Patricia15 Julai 2010

Hayo aliyaeleza wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Ntungamo.

https://p.dw.com/p/OJg5
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: dpa

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kuwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia kinahitaji kuongezwa kufikia wanajeshi 20,000 ili kupambana na kundi la wanamgambo la al-Shabaab lililodai kuhusika na mashambulio mawili ya mjini Kampala Jumapili iliyopita na kuwaua watu 74.

Rais Museveni aliyasema hayo jana usiku alipozungumza na waandishi habari katika wilaya ya Ntungamo, Magharibi mwa Uganda. Amesema Uganda inaweza kuchangia kukiimarisha kikosi hicho na kufikia wanajeshi 20,000 kitakachoshirikiana na serikali ya mpito ya Somalia kuwaondoa magaidi. Siku ya Jumatatu, kundi la al-Shabaab lilikiri kuhusika na mashambulio mawili ya mabomu yaliyotokea kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala na kuwaua watu 74 walipokuwa wakitazama fainali za mashindano ya Kombe la Dunia.

Rais Museveni alisema kuwa mataifa ya Afrika Mashariki tayari yalikuwa yamekubaliana kupeleka wanajeshi wa ziada 2,000 nchini Somalia, lakini baada ya mashambulio ya Jumapili iliyopita mjini Kampala, kikosi hicho kinatakiwa kuimarishwa zaidi. Kuna takriban wanajeshi 6,000 wa kulinda amani wa Afrika nchini Somalia, ikiwa ni pungufu ya wanajeshi wanaohitajika ambao ni 8,100. Kikosi hicho kinasaidia kuilinda serikali ya mpito inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi.

Rais Museveni alisema kuwa idadi hiyo ya wanajeshi kama walivyokubaliana mjini Addis Ababa, Ethiopia, itaongezwa, ingawa hawajakubaliana ni idadi gani ya wanajeshi Uganda itapeleka, lakini mataifa ya Afrika Mashariki yalikubali kwa sasa kupeleka wanajeshi 2,000 na baadaye wanajeshi 20,000. Aliongeza kusema kuwa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika watakapokutana, ndipo wataamua jinsi ya kulishughulikia suala hilo.

Kiongozi huyo wa Uganda amesema kuwa mashambulio ya Kampala yanaifanya nchi hiyo kutathmini upya uwepo wake kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Alisema wanajeshi wa Uganda wako mjini Mogadishu kwa ajili ya kuilinda bandari, uwanja wa ndege na Ikulu, lakini sasa wanamgambo wameifanya Uganda kuanza kukabiliana nao na kwamba watapambana na wale wote waliohusika na mashambulio hayo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Ndani nchini Uganda, Matia Kasaija amesema kuwa mripuaji mmoja alijitoa mhanga katika moja ya mashambulio mawili ya Kampala. Amethibitisha kuwa mwanamgambo mmoja alijiripua katika mkahawa wa Kiethiopia huko Kabalagala, kusini mwa Kampala. Aidha, msemaji wa polisi nchini Uganda, Judith Nabakooba amesema kuwa watuhumiwa sita wa mashambulio hayo wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano. Al-Shabaab walisema mashambulio hayo ni kulipiza kisasi kutokana na Uganda kuwa na wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia. Uganda ilikuwa ya kwanza kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia, mwanzoni mwa mwaka 2007.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman