Rais Salva Kiir amfuta kazi waziri wake wa fedha
16 Machi 2024Kufukuzwa kwa waziri, Bak Barnaba Chol, kulitangazwa katika televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Pauni ya Sudan Kusini ilipoteza karibu nusu ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani hali iliyochochea kupanda kwa bei ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.
Soma pia: Wabunge Sudan Kusini wamshutumu Kiir kukiuka makubaliano ya amani
Chol, mwenye umri wa miaka 43, na mshirika wa Rais Salva Kiir, aliteuliwa kuwa waziri wa fedha mwezi Agosti mwaka uliopita na alifanya mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa majina ya wafanyakazi hewa katika daftari la serikali na pia kuziba njia za kuvujisha mapato ya serikali.
Rais Kiir amemteua Awow Daniel Chuong, waziri wa zamani wa mafuta ya petroli, kuwa waziri mpya wa fedha.
Kadiri mzozo wa uchumi wa nchini Sudan Kusini unavyozidi kuongezeka, baadhi ya watumishi wa umma hawajapata mishahara kwa muda wa miezi sita sasa.