1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

090112 Guinea-Bissau Sanhá

Mohammed Khelef10 Januari 2012

Rais wa Guinea-Bissau, Malam Bacai Sanha, aliyefariki dunia hapo jana (9 Januari 2012) akiwa matibabuni Ufaransa, atakumbukwa kwa juhudi zake za kuipatia utulivu wa kisiasa nchi yake, ambayo jeshi lina usemi wa juu.

https://p.dw.com/p/13gmi
(100925) -- NEW YORK, Sept. 25, 2010 () -- Guinea-Bissau's President Malam Bacai Sanha addresses the general debate of the 65th session of the UN General Assembly at the U.N. headquarters in New York, the United States, on Sept. 25, 2010. (/Shen Hong) (lr)
Malam Bacai SanhaPicha: picture alliance/Photoshot

Sanha atakumbukwa kama raisi aliyetumia muda mwingi madarakani akiwa nje ya nchi kutafuta matibabu, lakini pia hatasahauliwa kwa dhamira yake ya kuikwamua nchi hiyo kutoka dimbwi la ufisadi, utawala mbovu na kupunguza nguvu kubwa za jeshi. Daima alisisitiza matumizi ya mazungumzo katika utatuzi wa migogoro.

"Ikiwa tunataka kuishi kwa amani, hatuwezi kutumia silaha kutatua matatizo yetu. Ni lazima tutumie nguvu za hoja kutatua matatizo yanayotukabili." Aliwahi kusema kiongozi huyo aliyefariki akiwa na miaka 64.

Sanha alizaliwa tarehe 5. Mei 1947 katika mji wa Quinará kusini magharibi mwa Guinea-Bissau akitokea kabila dogo la Waislamu liitwalo Beafada. Tangu udogo wake, alikuwa anapenda siasa, kwani mwaka 1962 alijiunga na chama cha kupigania uhuru wa Guinea-Bissau na Cape Verde (PAIGC). Chama hicho kilianzisha mapambano ya silaha dhidi ya ukoloni wa Kireno mwaka 1959.

Kama ilivyokuwa kwa wanachama wengi wa PAIGC, Sanha pia alikwenda kwenye nchi za iliyokuwa Ulaya ya Mashariki, ambapo alisoma Sayansi ya siasa na Uchumi katika chuo kikuu cha Karl Marx, huko Ujerumani ya Mashariki.

Muda mfupi baada ya kutambulika rasmi kwa uhuru kutoka kwa Ureno, hapo tarehe 10 Septemba 1974, Sanha alianza kazi kama afisa wa ngazi ya juu serikalini, kwanza kama mkuu wa utawala kwenye mkoa wa pwani wa Biombo na baadaye kama gavana wa mkoa wa Gabu. Katika vipindi tafauti, akawa pia waziri katika serikali ya Rais João Bernardo "Nino" Vieira.

Waziri Mkuu wa Guinea-Bissau, Carlos Gomes.
Waziri Mkuu wa Guinea-Bissau, Carlos Gomes.Picha: AP

Kufuatia kumalizika kwa "Vita Baridi" na pia shinikizo la wafadhili wa Magharibi, Guinea-Bissau nayo ikabadilisha mfumo wa siasa na kuanzisha wa vyama vingi. Katika uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1994, ambao ulimpa ushindi mkubwa Rais Nino Viera na chama chake cha PAIGC, Sanha akachaguliwa kuwa spika wa bunge kwa miaka mitano, kutoka mwaka 1994 hadi 1999.

Mwaka 1998, hata hivyo, kukafanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi chini ya uongozi wa mkuu wa majeshi, Ansumane Mane, na nchi ikaingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Katika kipindi hicho, Sanha akiwa kama spika wa bunge, akachukuwa nafasi ya raisi wa muda. Mwaka 2000 akajaribu kwa mara ya kwanza kugombea nafasi ya uraisi lakini akashindwa na Kumba Yala, ambaye naye akaondoshwa baadaye kwa mapinduzi ya kijeshi yasiyo umwagaji damu. Mwaka 2005, Sanha akajaribu tena kugombea uraisi, na mara hii akashindwa katika duru ya pili na raisi wa zamani, Nino Vieira.

Kuanzia mwaka 2009, Guinea-Bissau ikaingia tena kwenye machafuko baada ya Rais Nino Vieira kuuawa na saa chache baadaye kuuawa pia kwa mkuu wa majeshi, Batista Tagme Na Waie kuuawa. Hadi sasa haijafahamika waliofanya mauaji hayo. Mara hii Sanha akashinda uchaguzi katika duru ya pili kwa zaidi ya asilimia 60, akichaguliwa kutokana na ahadi yake ya kuiunganisha nchi.

Aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Guinea-Bissau, Zamora Induta
Aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Guinea-Bissau, Zamora IndutaPicha: picture alliance/dpa

"Nitafanya kila linalowezekana, ili taasisi za dola zilizoanzishwa na katiba na sheria zifanye kazi. Ninataka kujenga mazingira ya kufanya kazi pamoja, kati ya serikali, bunge na vyombo vya mamlaka ya nchi." Alitoa kauli hii wakati akiapishwa.

Lakini hata chini ya utawala wa Sanha, Guinea-Bissau haijafaidi amani ya kweli. Mwezi Aprili mwaka 2010 wanajeshi wanaomtii mkuu wa zamani wa majeshi, Zamora Induta, waliasi na pia kuishambulia kwa saa kadhaa ofisi ya waziri mkuu, Carlos Gomes. Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana, kuifanyika jaribio jengine la mapinduzi ya kijeshi.

Karibuni majaribio yote yalimkuta Malam Bacai Sanha akiwa hospitalini mjini Paris, Ufaransa. Kwa miezi kadhaa nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na waziri mkuu wake, wakati yeye akitafuta matibabu nje ya nchi. Haijulikani hadi sasa ni ugonjwa gani hasa uliokuwa ukimsumbua, lakini uvumi unasema alikuwa na maradhi ya kisukari.

Kifo chake, hapa shaka, kinazua wasiwasi wa kugombania madaraka, katika nchi hiyo iliyozowea mapinduzi ya kijeshi na mauaji ya viongozi wakuu wa serikali. Kwa sasa, hata hivyo, spika wa bunge, Raimundo Pereira, ndiye anayeshikilia uraisi wa muda.

Ulaya itamkumbuka Sanha kwa makubaliano yaliyokiruhusu kikosi cha wanajeshi wa Angola kupiga kambi mjini Bissau, kwa lengo la kutoa mafunzo jeshi la nchi hiyo kukabiliana na magenge ya madawa ya kulevya ya Amerika Kusini, yanayoitumia Guinea-Bissau kama kituo cha kusafirishia madawa barani Ulaya. Mafanikio ya vita hivi yangeliweza kuwa zawadi pekee ambayo marehemu Malam Bancai Canha angeliwaachia raia wake.

Mwandishi: Helena de Gouveia
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo