Tshisekedi amekutana na mtangulizi wake kujadili mivutano
22 Septemba 2020Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,Felix Tshisekedi amefanya mkutano wa nadra na mtangulizi wake Joseph Kabila katika kipindi ambacho wafuasi wa Kabila,wanasema kwamba anaweza kurejea katika ulingo wa kisiasa. Mkutano huo umefanyika huku mvutano baina ya washirika hao wawili ukiwa unashika kasi.
Ni kwa mara ya kwanza viongozi hao wawili kukutana katika miezi ya hivi karibuni. Bado kumekuwa na hali ya vuta ni kuvute baina ya chama cha FCC cha Joseph Kabila na kile cha UDPS cha rais Tshisekedi.
Duru kutoka pande zote mbili, zinaelezea kwamba Tshisekedi na Kabila walijadiliana kuhusu maendeleo ya muungano unaongoza serikali. Lakini hakukutolewa taarifa zaidi kufuatia kikao hicho kilichodumu muda wa masaa kadhaa.
Muungano FCC- CACH wakumbwa na mivutano
Mvutano wa kisiasa uliibuka mwezi Juni baada ya Rais Tshisekedi kuteuwa viongozi wapya wa jeshi na majaji wa korti ya katiba bila mashauriano ya awali na waziri mkuu ambaye ni kutoka chama cha FCC cha Kabila. Chama cha FCC kinamlaumu pia rais Tshisekedi kwa kutomteua waziri mpya wa sheria kutoka chama hicho miezi mitatu baada ya kujiuzulu kwa waziri Tunda ya Kasende kufuati tofauti zake na rais Tshisekedi. Kuteuliwa kwa mwenyekiti mpya wa tume huru ya uchaguzi kumevigawanya pia vyama hivyo viwili. Chama cha FCC chenye viti vingi bungeni kiliridhia jina la Ronsard Malonda kama mwenyekiti mpya wa tume ya uchaguzi,lakini rais Tshisekedi alitakaa kuidhinisha uteuzi huo na kuomba kuweko na mchakato mpya.
Chama cha FCC kilielezea wazi kwamba hatua kadhaa za rais Tshisekedi zimekiuka katiba.
Delphin kapaya,mchambuzi wa maswala ya Kongo amesema kwamba mkutano wa viongozi hao wawili ni kujaribu kuzima moto wa kisiasa.
Kwa upande wake chama cha UDPS cha rais Tshisekedi kimesema washirika wao serikalini kutoka chama cha FCC cha Kabila hawana nia nzuri. Augustin Kabuya, katibu mkuu wa chama hicho ameiambia DW kwamba maafisa wa FCC wamefanya juu chini ili rais Tshisekedi ashindwe katika muhula wake wa uongozi.
Kabila kurejea madarakani 2023?
Kwenye taarifa iliotolewa na gazeti la kila wiki la Ufaransa, Jeune Afrique ni kwamba mkataba wa siri baina ya Kabila na Tshisekedi baada ya uchaguzi wa Desemba 2018 ni kwamba baada ya muhula wa miaka mitano rais Tshisekedi anatakiwa kumuunga mkono mgombea kutoka chama cha FCC cha Kabila. Chama cha UDPS kimetupilia mbali madai hayo na kusema mgombea wake kwenye uchaguzi wa 2023 ni Tshisekedi.
Hivi karibuni maafisa wa chama cha FCC cha Kabila wamesema kwamba wameanza kulifanyia kazi suala la Kabila kurejea katika kiti cha urais, mchakato ambao unatarajiwa kufanyika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Mbunge kutoka chama hicho, Alphonse Ngoy Kasanji amesema wamefikiria mabadiliko ya katiba ili rais achaguliwe na bunge na sio moja kwa moja na raia.
Rais Kabila ambaye alidumu madarakani kwa takribani miaka 18 amekuwa kimya katika kipindi kirefu na kwa kiasi kikubwa amekuwa akijiepusha kuonekana hadharani.