1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kenyatta awahimiza wanawake kujitosa katika biashara

11 Februari 2021

Viongozi na wakuu wa Umoja wa Afrika wamewahimiza wanawake barani Afrika kujitosa katika sekta ya biashara ili kunufaika ipasavyo na mpango wa bara hilo kuwa kanda ya biashara huru.

https://p.dw.com/p/3pEGI
Kaverdische Inseln
Picha: dpa

Kwenye kikao maalum kilichofanyika kwa njia ya mtandao kujadili hali ya biashara miongoni mwa mataifa ya Kiafrika, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa mwito kwa wadau barani humo kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika shughuli za biashara.

Hata hivyo, wanawake wengi bado wanahisi kuwa kuna changamoto si haba kutokana na dhuluma za kijinsia.

Aidha Rais Kenyatta amesema kuwa yeye yumo kwenye mstari wa mbele katika kuwapigia debe wanawake wafanyabiashara barani Afrika. Naye katibu mkuu wa Tume ya Uchumi barani Afrika Bi. Vera Songwe, ambaye ni mchumi kutoka Cameroon, amewahimiza viongozi na wadau barani Afrika kufanya kila jitihada kufanikisha nafasi za biashara miongoni mwa wanawake hasa katika sekta ya ubunifu na teknolojia ya kisasa.

Kwenye mkutano huo, wasemaji walipigia upatu mpango wa bara la Afrika kuwa kanda ya biashara huru, ambao unalenga kuwaunganisha watu bilioni 1.3 barani humu sawia na kuunda soko jipya la kiuchumi lenye thamani ya kiasi cha dola trilioni 3.4.