1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAngola

Rais wa Angola amsamehe mtoto wa mtangulizi wake

26 Desemba 2024

Rais wa Angola Joao Lourenco amewasamehe wafungwa 50, akiwemo mtoto wa kiume wa mtangulizi wake Jose Eduardo dos Santos. Jose Filomeno dos Santos, alikuwa akitumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la ubadhirifu.

https://p.dw.com/p/4oawu
Rais wa Angola Joao Lourenco
Rais wa Angola Joao Lourenco amewasamehe wafungwa 50, akiwemo Jose Filomeno dos Santos. Picha: Adrian Dennis/AFP/AP/picture alliance

Amri ya rais iliyoandikwa kwenye Facebook ilitaja "tabia nzuri" na "kutokuwepo na hatari yoyote kwa jamii" kama sababu zilizowapa uhuru wafungwa hao.

Soma pia: Binti wa dos Santos anakabiliwa na kesi mahakamani

Jose Eduardo dos Santos, aliyefariki mwaka wa 2022, aliitawala Angola ambayo ina utajiri wa nishati, kwa miaka 38 hadi mwaka wa 2017. Mtoto wake Jose Filomeno dos Santos alifungwa jela 2020 baada ya dola milioni 500 kuhamishwa kutoka benki ya taifa ya Angola hadi kwenye akaunti moja nchini Uingereza.

Watu wengine watatu, akiwemo gavana wa zamani wa benki ya taifa ya Angola, walifungwa jela. Ilikuwa hukumu kubwa kabisa ya ufisadi kutolewa Angola tangu mapokezano ya madaraka. Mwezi Novemba, serikali ya Uingereza ilimuwekea vizuizi Isabel dos Santos, mfanyabiashara bilionea na binti ya Dos Santos, kama sehemu ya kampeni mpya ya kupingwa rushwa.