1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Armenia aidhinisha uamuzi wa kujiunga na ICC

14 Oktoba 2023

Rais wa Armenia Vahagn Khachuryan ameidhinisha uamuzi wa bunge wa kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, hatua ambayo imezidi kuzorotesha uhusiano wa nchi hiyo na mshirika wake wa zamani wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4XXX8
Niederlande, Den Haag | Internationaler Strafgerichtshof
Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Wiki iliyopita, bunge la Armenia lilipiga kura ya kutaka kujiunga na ICC kwa kuridhia Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo. Nchi ambazo zimetia saini na kuridhia Mkataba huo zinawajibu wa kumkamata Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye anatafutwa na ICC kwa madai ya uhalifu unaohusishwa na kuwasafirisha watoto kutoka nchini Ukraine.

Soma pia: Mzozo wa Nagorno-Karabakh wafika mahakama ya haki, ICJ

Mwezi uliopita Moscow ilikosoa hatua ya Armenia ya kutaka kujiunga na ICC na kuitaja kama "hatua isiyo ya kirafiki lakini Armenia baadaye iliihakikishia Urusi kwamba Putin hatakamatwa iwapo ataingia nchini humo.

Mjumbe wa Armenia kuhusu masuala ya kisheria ya kimataifa, Yegishe Kirakosyan, alisema Yerevan iliamua kurejesha mchakato wa kujiunga na ICC kwa sababu ya hatua zinazodaiwa za Azerbaijan dhidi ya Armenia.