Rais wa Iran alaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Houthi
15 Januari 2024Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Iran, IRNA, likinukuu mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Raisi na kiongozi mkuu wa waasi wa Houthi wa nchini Yemen, Mahdi al-mashat.
Akizungumzia mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za Wahouthi nchini Yemen, Raisi amesema hayo ni matendo "yanayopingwa na kulaaniwa na nchi zote zinayopendelea uhuru duniani."
Washington imekuwa ikizilenga ngome za waasi Houthi kwa kile viongozi wa Marekani wanasema kurejesha usalama kwenye njia muhimu ya biashara kwenye Bahari Nyekundu.
Waasi hao wamekuwa wakizilenga meli za mizigo kwa makombora na droni kwa lengo la kuishinikiza Israel isitishe kampeni ya kijeshi huko Gaza.
Kiongozi wa Iran amemweleza Al-Mashat kwamba kuwaunga mkono Wapalestina "wasio na nguvu" ni msimamo usioyumba wa Iran.