1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAngola

Rais wa Marekani Joe Biden aelekea ziarani Angola

Angela Mdungu
2 Desemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ameelekea nchini Angola katika moja ya ziara zake za mwisho kimataifa kabla ya kuachia kiti cha Urais. Biden, hakuchagua kuitembelea Angola kwa bahati mbaya.

https://p.dw.com/p/4ndma
Joe Biden ameelekea ziarani Angola
Rais wa Marekani Joe Biden alipotembelewa na Rais wa Angola Joao Manuel Goncalves Lourenco mjini Washington Novemba 30, 2023 Picha: Yuri Gripas/ABACAPRESS/picture alliance

Mnamo mwezi Oktoba, Biden aliahirisha mpango wa kuitembelea Angola wakati Kimbunga Milton kilipokaribia kulifikia jimbo la Florida. Alifanya hivyo ili kusimamia mipango ya kukabiliana na janga hilo.

Katika ziara ya sasa, mara tu atakapotua mjini Luanda, atashughulikia ajenda kadhaa. Anatarajiwa kutia saini mikataba ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi ikiwa ni ishara ya kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Angola. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Claudio Silva anasema ziara hiyo ni mafanikio makubwa kwa Angola.

Soma zaidi:Rais Biden aanza ziara ya siku mbili nchini Angola 

Kufanyika kwa ziara ya Biden, muda mfupi baada ya uchaguzi wa Marekani siyo jambo linalotokea kwa bahati mbaya na kutambuliwa kwa miradi ya ushirikiano kunaonekana kupewa kipaumbele

Angola ina miradi muhimu ya sasa na ya baadaye inayoihusisha Marekani iliyotoa mkopo kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa mtambo wa kusafisha mafuta wa Soyo kaskazini mwa Angola. Pia ina mradi wa reli wa Lobito ambao ndiyo mkubwa zaidi. Mradi huo wa reli unaiunganisha bandari ya Lobito katika Pwani ya Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia yenye utajiri wa Madini.

Ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Angola wazidi kukua

Wakati ziara hiyo ya Biden ikitarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kijeshi, mwanasosholojia Paulo Ingles aliyewahi kufanya utafiti katika chuo cha jeshi cha Munich na Bayreuth anasema kwa sasa ushirikiano katika sekta hiyo kati ya Marekani na Angola umekua. Ingles anasema kuwa  Marekani inapanga kujenga kambi ya kijeshi Kaskazini mwa Angola kwani hatua hiyo itaendana na maslahi ya kimkakati ya kijiografia ya Marekani.

Lobito, Angola
Wafanyakazi wa reli ya Benguela nchini AngolaPicha: Liu Zhi/Photoshot/picture alliance

Soma zaidi: Biden akutana na kiongozi wa Angola huku Marekani ikilenga kukabiliana na China barani Afrika

Mtaalamu wa diplomasia ya Kimataifa wa Angola Kinkinamo Tussamba ameiambia DW kuwa, kwa hakika ziara ya Biden nchini Angola ni tukio la Kihistoria lakini kwa bahati mbaya haiwezi kubadilisha maisha ya Waangola kuwa bora zaidi.

Tussamba anabainisha kuwa huenda ni kundi dogo la watu wenye hadhi ya juu wa nchini humo ndiyo pekee watakaonufaika na uwekezaji wa Marekani, kama ilivyokuwa kwa miradi mikubwa ya Wachina iliyofanywa Angola na si vijana wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya ajira.