1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Rais wa Nigeria atoa wito wa kusitishwa kwa maandamano

5 Agosti 2024

Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ametoa wito wa kusitishwa kwa maandamano nchini humo yanayopinga gharama ya juu ya maisha na kusema maandamano hayo yamegeuka kuwa vurugu na kuwalaumu watu wachache wenye ajenda ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/4j7Wq
Waandamanaji wafanya maandamano mjini Lagos kupinga kupanda kwa gharama ya maisha mnamo Agosti 2, 2024
Maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha nchini NigeriaPicha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Katika hotuba iliyorushwa kupitia televisheni, Rais Tinubu aliwataka waandamanaji hao kusitisha maandamano yoyote zaidi na kutoa nafasi ya mazungumzo, haya yakiwa matamshi yake ya kwanza ya umma tangu kuanza kwa maandamano hayo.

Rais Tinubu anasema anaelewa matatizo ya wananchi

Rais huyo amesema amewasikia waandamanaji kwa sauti kubwa na wazi, na kuongeza kuwa anaelewa mafadhaiko yanayochochea maandamano hayo huku akiwahakikishia wananchi serikali yake imejitolea kusikiliza na kushughulikia wasiwasi wao.

Rais Tinubu akosolewa na baadhi ya watu

Matamshi ya kiongozi huyo yalikosolewa na baadhi ya watu waliosema ameshindwa kushughulikia masuala yaliyosababisha maandamano hayo.

Soma pia:Rais Tinubu aahidi kushughulikia kero za raia wa Nigeria

Katika tathmini yake, kampuni ya utafiti wa kijasusi ya SBM yenye makao yake mjini Lagos, imesema kuwa ilikuwa fursa iliyopotezwa ambapo kiongozihuyo wa Nigeria alijiepusha na masuala ya msingi na kukosa kutoa muongozo ama malengo ya wazi ya kukabiliana nao.

Vikosi vya usalama vyashtumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi

Maandamano hayo yaliyoanza siku ya Alhamisi, yameambatana na ripoti za uporaji na uharibifu, pamoja na shutuma kwamba vikosi vya usalama vimetumia nguvu kupita kiasi.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limeripoti vifo vya waandamanaji tisa katika makabiliano na polisi, huku wengine wanne wakiuawa kwa bomu.

Maafisa wa polisi warusha vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Abuja nchini Nigeria mnamo Agosti 1 2024.
Maafisa wa polisi wawatawanya waandamanaji nchini NigeriaPicha: Kola Sulaimon/AFP

Hata hivyo, polisi ya Nigeria imekanusha ripoti hiyo ya Amnesty International.

Soma pia:Watu 13 wauawa katika siku ya kwanza ya maandamano Nigeria

Maandamano hayo yanaonyesha mafadhaiko kutokana na mzozo mbaya zaidi wa gharama ya juu ya maisha na tuhuma za ubadhirifu na ufisadi katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika ambayo pia ni mzalishaji mkuu wa mafuta ambapo mapato ya umma yanatofautiana na viwango vya juu vya umaskini na njaa.

Wasaidizi wa Tinubu wanasema maandamano yamechochewa kisiasa

Wasaidizi wa Tinubu wanasema maandamano hayo yamechochewa kisiasa. Uchaguzi wake mwaka jana ulipingwa na upinzani, baada ya kushinda kwa 37% ya kura, idadi ndogo zaidi ya rais yeyote wa Nigeria kuwahi kushuhudiwa.

Soma pia:Polisi Nigeria wafyatua gesi ya machozi kutawanya waandamanaji

Uchaguzi huo pia ulirekodi idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura tangu 1999, wakati nchi hiyo iliporejea kwenye mfumo wa demokrasia.

Waandamanaji hao pia wametiwa moyo na vijana wengine nchini Kenya waliofanya maandamano mwezi uliopita kupinga mpango wa nyongeza ya kodi.