Rais wa Senegal Macky Sall avunja serikali
7 Oktoba 2023Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais, Waziri Mkuu Amadou Ba, ambaye ni mrithi mteule wa Sall kama mgombea urais wa muungano unaotawala, ndiye pekee aliyesalia katika nafasi ya uongozi kwa sasa.
Muundo wa serikali mpya nchini humo unatarajiwa kutangazwa tena hivi karibuni. Baada ya maandamano na ghasia Sall, mwanasiasa wa mrengo wa kati ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya muongo mmoja, alitangaza kutowania muhula wa tatu ulio na utata.
Wagombea kadhaa wa Urais wanatafuta idadi ya wafuasi inayokubalika kisheria ili kuidhinishwa kuwa wagombea halali.
Hayo yanajiri wakati ambapo mwanasiasa kinara wa upinzani Ousmane Sonko, alishaondolewa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo, baada ya kuhukumiwa kifungo katika kesi ya unyanyasaji.
Takriban raia milioni 17 wa Senegal wanatarajiwa kumchagua kiongozi mpya wa serikali yao Februari 25 mwakani.