Rais wa Somalia ataka kurejeshwa mezani mjadala wa uchaguzi
28 Aprili 2021Uamuzi huo pia unatokana mapigano ya mjini Mogadishu, ambayo yamevigawa vikosi vya usalama kwa misingi ya kikabila. Katika hotuba yake Rais, Abdullahi Mohammed maarufu kama Farmajo ameyalaumu matiafa ya kigeni kwa kuchochea vurugu. Na pia kuwatuhumu wanasiasa wanaotumia damu ya vijana wa Kisomali katika kujitafutia madaraka.
Aidha katika hotuba yake hiyo kwa taifa alisema anaunga mkono jitihada ya waziri mkuu na viongozi wengine wa kisiasa na kuunga mkono hasa suala la kufanyika kwa uchaguzi. Hata hivyo rais huyo hakujiuzulu kama ilivyotarajiwa na wengi, lakini amesema atazungumza na bunge Jumamosi kwa lengo la kulipa taarifa ya maendeleo ya kisiasa nchini humo.
Rais Abdullah aonesha nia ya wazi wa kufanyika kwa uchaguzi wa haraka.
Kwa sasa Rais Abdullah anaonesha kuwa tayari na kuendelea na uchaguzi, wenye kujikita katika makubaliano ya Septemba 17, ambayo yalihusisha serikali yake na viongozi wa majimbo ambao umekuwa ukisisitizwa na jumuiya ya kimataifa.
Rais huyo alikuwa kimya tangu mamia ya wanajeshi kujitokeza hadharani katika viunga vya mji mkuu Mogadishu na kupinga mamlaka yake, mkasa ambao ulizusha machafuko na vikosi vya usalama na kuzusha miito ya amani ya jumuiya ya kimataifa.
Baadhi ya raia wa Somalia walianza kuitoroka nchi hiyo kwa kuhofia usalama wako baada ya kipindi cha miaka kadhaa ya jitihada ya kulijenga upya taifa hilo. Katika kipindi kifupi cha vuta nikuvute mamlaka za majimbo ya Hirshabelle na Gamudug yalibadili msimamo na kutaka dhidi ya rais na kutaka kurejesha meza ya mazungumzo kuhusu uchaguzi, ambao awali ulipaswa kufanyika mapema Februari.
Waziri Mkuu Mohammed Hussein Roble, aliunga mkono taarifa hiyo ya pamoja na kuvitolea wito vikosi vya usalama kurejea makambini. Na kutaka Somalia irejee katika meza ya mazungumzo, huku akiwataka pia viongozi wa kisiasa kuacha vitendo vyoyote ambavyo vinaweza kuathiri hali ya usalama wa taifa hilo kwa sasa.
Uchaguzi nchini Somalia umekuwa ukicheleweshwa kwa mara kadhaa kutokana na tofauti zilizopo kati ya serikali ya shirikisho na majimbo ya Puntland na Jubaland sambamba wanasiasa wa upinzani.
Vyanzo: DPA/AFP