1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Yoweri Museveni afungia Facebook nchini Uganda

13 Januari 2021

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameifungia Facebook nchini humo akiishtumu kwa kuonyesha kuwa ina hila dhidi ya utawala wake.

https://p.dw.com/p/3nqM7
Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Wahlplakate
Picha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Akihutubia taifa Jumanne jioni saa chache  baada ya muda wa kampeni kumalizika, Rais Museveni ameonya kuwa yeyote atakayeshiriki vitendo vya wizi wa kura atakuwa anafanya kitendo cha uhaini.

Rais Museveni amesema utawala wake umechukua hatua ya kuifungia Facebook nchini Uganda kama hatua ya kulipiza kisasi kwa kitendo cha kampuni hiyo ya kimataifa kuwafungia wafuasi wa chama tawala NRM.

Soma pia: Wanaharakati wa haki za binadamui wahofia usalama wao Uganda

Kulingana na Facebook waliamua kufunga majukwaa ya watu waliokuwa wakienda kinyume na sera ya kampuni hiyo kuhusu maadili. Angalau watumiaji 100 wa Facebook walio na mafungamano na chama cha NRM waliathirika kutokana na hatua hiyo.

Sambamba na tangazo la Museveni kufungia Facebook, kamatakamata ya wanahabari wa mtandaoni wanaohusishwa na mgombea urais wa chama cha NUP Robert Kyagulanyi imeripotiwa. Lakini baadhi ya wanahabari hao walio mafichoni wameapa kuendelea kuelezea ulimwengu kile kinachoendelea Uganda.

Uganda | Opposition | Bobi WIne
Picha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture alliance

Siku kadhaa zilizopita, wanasiasa wa upinzani walitoa tahadhari kwa wananchi kwamba serikali ilikuwa na mpango wa kuifungia mitandao ya kijamii na kwa jumla kutatiza huduma za intaneti.

Soma pia: Je uchaguzi utakuwa wa huru na haki?

Waliochukua tahadhari waligeukia matumizi ya app mbadala  kama vile VPN kuepukana na usumbufu huo. Mitandao ya kijamii ilitarajiwa kuwezesha mawasiliano kutoka sehemu mbalimbali za nchi ili matokeo ya uchaguzi yafahamike mubashara.

Mtaalamu wa teknolojia na habari Albert Mucunguzi ametaja hatua ya Uganda kuifungia Facebook kuwa kinyume kabisa na mchakato wa kuwezesha uhuru wa kujieleza ambao ni haki ya binadamu.

Katika hotuba yake kwa taifa ikiwa imesalia saa chache uchaguzi mkuu kufanyika, Rais Museveni ametoa onyo kali kwa yeyote atayejaribu kushiriki vitendo vya wizi wa kura. Amataja vitendo hivyo kuwa vya kihaini.

Museveni amekariri kuwa usalama umeimarishwa kote nchini na hakuna visa vyovyote vya kuvuruga zoezi la uchaguzi vitatokea.

Mwandishi; Lubega Emmanuel DW Kampala.