RB Leipzig bado yaonesha ubabe
23 Januari 2017Katika ligi ya Ujerumani Bundesliga , Bayer Leverkusen imeanza vizuri mzunguko huu wa pili wa Bundesliga kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Hertha BSC Berlin jana Jumapili . Bayer Leverkusen ilishinda jana baada ya michezo mitatu ya nyumbani mfululizo bila ushindi na sasa inamatumaini ya kupanda na kushika moja kati ya nafasi za kuweza kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao. Bayer Leverkusen imejikusanyia hadi sasa pointi 24 ikishika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi. Kocha wa Leverkusen Roger Schmidt anasema,
„Kwa kweli hatukucheza vizuri sana. Lakini hilo halikutarajiwa. Kuna mambo machache yaliyofanyakazi, ambayo yalitosha kuweza kushinda. Tulifanya mambo machache vizuri , na pia upo uwezo wa kufanya vizuri zaidi. Lakini msingi ulikuwapo. Nimeiona timu yangu , kuwa ina uwezo mkubwa. Ndio sababu nimefurahishwa."
Katika mchezo mwingine jana wa kukamilisha duru ya michezo 17 ya mzunguko wa kwanza wa Bundesliga msimu huu , FC Koln ilipoteza fursa ya kujipenyeza katika nafasi za kucheza katika ligi ya Ulaya msimu ujao baada ya kutoka sare tasa na Mainz 05.
Siku ya Jumamosi, RB Leipzig ilifanikiwa kung'ang'ania kileleni mwa ligi baada ya kuirarua Eintracht Frankfurt kwa mabao 3-0 na kujiweka pointi tatu tu nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich, ambapo Bayern sasa ina pointi 42 baada ya kuishinda Freiburg siku ya Ijumaa kwa mabao 2-1. Borussia Dortmund ambayo imemsajili leo kijana wa miaka 17 raia wa Sweden Alexander Izak kwa kitita cha euro milioni 10 ilipata ushindi wa kibarua kigumu dhidi ya Werder Bremen wa mabao 2-1.
Hoffenheim ni timu pekee katika ligi kuu za bara la Ulaya ambayo hado haijaonja kipigo hadi sasa, na siku ya Jumamosi ilionesha kuwa inaweza kurefusha rekodi hiyo kwa kuikandika Augsburg kwa mabao 2-0. Hoffenheim inaikaribisha Leipzig wiki hii katika pambano ambalo tayari linasubiriwa kwa hamu. Kocha wa Hoffenheim akizungumzia ushindi wa timu yake dhidi ya Augusburg, alisema.
"Kwa msingi wa kipindi cha pili tulistahili kushinda. Tulicheza kidogo kwa tahadhari zaidi. Kwa mtazamo wangu katika kipindi cha kwanza tuliweka tahadhari mno, tulicheza kwa kumiliki mpira mno. Hali hiyo kwangu ilinikera kidogo."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahhman