1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ricciardo ampiku Rosberg katika Canada GP

9 Juni 2014

Daniel Ricciardo wa kikosi cha Red Bull alishinda kwa mara ya kwanza kabisa mashindano ya mbio za magari ya Formula One katika mkondo wa Canada Grand Prix, na kuipunguza kasi ya timu ya Mercedes.

https://p.dw.com/p/1CEys
Formel 1 Grand Prix Kanada 08.06.2014
Picha: Reuters

Dereva huyo wa timu ya Red Bull alipata ushindi wake wa kwanza kabisa wa Formula One na wa kwanza kwa dereva mwingine mwaka huu kando na Nico Rosberg na Lewis Hamilton. Ricciardo alimpiku Rosberg, anayeongoza katika msururu wa madereva, na aliyeanza katika nafasi ya kwanza katika mbio za jana mjini Montreal, ikiwa imesalia mizunguko miwili mbio hizo kukamilika. Hamilton alilazimika kuyaaga mashindano hayo katika mzunguko wa 48 kutokana na matatizo ya breki.

Rosberg alimaliza katika nafasi ya pili, na kuutetea uongozi wake katika msimamo wa ubingwa wa dunia. Mjerumani huyo ana pointi 140 baada ya mikondo saba ya mashindano hayo msimu huu, kwa kushinda mara mbili na kumaliza katika nafasi ya pili katika mashindano matano.

Hamilton bado anashikilia nafasi ya pili katika msururu huo akiwa na pointi 118. Ricciardo alisonga katika nafasi ya tatu akiwa na pointi 79, baada ya kumpiku Fernando Alonso wa timu ya Ferrari ambaye alimaliza katika nafasi ya sita katika mbio za jana na ana pointi 69.

Sebastian Vettel alipanda jukwaani katika nafasi ya tatu na kuikamilisha siku njema ya timu ya Red Bull. Riccardo huenda sasa anaondoka katika kivuli cha Vettel, bingwa mtetezi mara nne wa Formula One. Muaustralia huyo mwenye umri wa miaka 24, amepata nafasi ya nne katika mikondo miwili, nafasi mbili katika mikondo mitatu na ameshinda mara moja katika mbio tano zilizopita.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman