1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya hali ya maendeleo duniani

Sabine Ripperger / Maja Dreyer3 Novemba 2005

Mashirika ya kutoa misaada ya Ujerumani „Terre des Hommes“ na „Welthungerhilfe“ wameitaka serikali mpya ya Ujerumani kuongeza jitihada zake za kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Mashirika hayo yamesema hivyo wakati wa kutoa ripoti yao ya hali ya maendeleo duniani mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/CHeU
Wahanga wa Tsumani wanahitaji misaada ili kuanzisha tena maisha ya kujitegemea
Wahanga wa Tsumani wanahitaji misaada ili kuanzisha tena maisha ya kujitegemeaPicha: AP

Mwakilishi wa shirika la „Terre des Hommes“, Wolf Christian Ramm, alisema kuaminika serikali mpya itategemea pia kutimiza ahadi zao za misaada ya maendeleo pamoja na kutoangalia fedha za maendeleo katika zoezi lake la kupunguza bajeti ya mwaka ujao.

Ingawa Ujerumani imekubali kuongeza misaada ya maendeleo kufikia asimlia 0.7 ya pato la taifa mwaka 2015 kama ilivyopangwa na Umoja wa Mataifa, mpaka sasa misaada ya maendeleo inagharamia tu asilimia 0.3 ya pato la taifa la Ujerumani. Lazima serikali mpya ibadilishe mwenendo huo, alisema Bw. Ramm.

Pamoja ya hayo Bw. Ramm alisifu kuwa sekta ya elimu itapewa misaada zaidi, hata hivyo namna ya kusisitiza sekta fulani katika kutoa misaada inaonyesha kwamba malengo ya milenia hayapewi umuhimu wa kwanza.

Kwa mujibu wa Shirika la „Terre des Hommes“, siasa ya maendeleo na suala la mahusiano baina ya Kaskazini na Kusini mwa dunia yalipewa uangalifu wa pekee mwaka huu kutokana na tamasha kubwa za muziki duniani kote, ushirikiano wa kimataifa pamoja na watu wengi kutoa michango kuwasaidia wahanga wa Tsumani.

Bw. Ramm alisema serikali ya Ujerumani itabidi ihakikishe kwamba mambo ya maendeleo yanapewa umuhimu huo siku za usoni: „Sasa hivi tuna nafasi kubwa ya kuipa sifa ya kimataifa kwa kuchukua hatua madhubuti za kuongeza jitihada zake za kutoa misaada na kuonyesha malengo na kanuni zake nzuri. Lakini isiwe kama Waingereza wasemavyo, business as usual, yaani kazi ya kawaida, wala kuvunjika mambo ya maendeleo kwa kuyatumia kwa maslahi mbali mbali ya kisiasa.“

Karibu mwaka mmoja baada ya janga la Tsunami kutokea mashirika ya Terres des Hommes na Welthungerhilfe yametoa matokeo ya mchanganyiko kuhusu misaada iliyotolewa na serikali. Mkuu wa shirika la Welthungerhilfe, Bw. Hans-Joachim Preuß, aliihakiki serikali ya Ujerumani kwa kuyapa mashirika yasiyo ya kiserikali asilimia tano tu ya Euro bilioni 500 zilizotolewa kwa jumla. Jambo hilo haliwezi kufahamika kwa sababu mashirika haya yana uwezo mkubwa kuliko taasisi za kiserikali wa kuwasaidia wahanga. Lazima serikali mpya ya Ujerumani ineemeshe kazi yake.

Pamoja na hayo mashirika ya kutoa misaada yalijifunza mambo mengi kutokana na uzoefu wao huko Kusini Mashariki mwa Asia. Bw. Preuß alisema: „Ilionekana kwamba lazima tuangalie mbali na siyo tu kuleta misaada ya haraka ili kuwawezesha watu kujenga upya nchi zao. Badala ya kuondoa tu madhara tunabidi pia kuwapa watu misaada ya kuanza tena maisha ya kujitegemea. Vile vile ni lazima kuyashirikisha makundi yaliyopo kando mwa jamii mpaka sasa kwani kuwasaidia tu wahanga wa janga la tsunami itaongeza ubaguzi wa kijamii, jambo ambalo litaathiri sana nchi hizi.“

Mbali na Tsunami ya Asia, yalitokea majanga mengine duniani, kama kwa mfano ukame katika nchi za eneo la Sahel barani Afrika, vita nchini Sudan na tetemeko la ardhi nchini Pakistan.

Katika ripoti yao mashirika ya „Terre des Hommes“ na „Welthungerhilfe“ yamesema changamoto kubwa zaidi ya siasa ya mambo ya maendeleo ni kupambana na majanga haya yanayotokea duniani kote lakini hayakusikika sana kwenye vyombo vya habari. Kwa jumla Umoja wa Mataifa una orodha ya maeneo 20 yanayokabiliwa na majanga ya aina mbali mbali na yanahitaji misaada ya ukarimu.