1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Malengo ya Mailenia

Lillian Urio13 Aprili 2005

Kupunguza kwa nusu umasakini wa hali ya juu, kila mtoto kupata elimu ya msingi na kutokomeza UKIMWI na malaria - Haya ndio malengo matatu kati ya manane ambayo viongozi wa nchi mbalimbali waliamua kuyafikia katika mkutano wa Milenia wa Umoja wa mataifa, mwaka wa 2000. Hadi ufikapo mwaka 2015 malengo haya yanatakiwa yawe yametimizwa na umasikini uwe umepunguzwa. Benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa, IMF yametoa ripoti, itwayo Global Monitoring, inayochunguza jinsi malengo haya yalivyo tekelezwa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/CHh3
Nembo ya Shirika la fedha la kimataifa, IMF
Nembo ya Shirika la fedha la kimataifa, IMF

Ripoti hii ya Benki ya dunia na IMF imeonyesha kwamba lengo kuu la Mailenia la kupunguza umaskini wa hali ya juu kwa nusu, ifikapo mwaka 2015, linaweza kutimizwa.

Idadi ya watu, wanaoishi katika umasikini wa hali ya juu, itapungua kwa nusu kutokana na China na India. Hii ni kwa sababu ya kuboreka kwa hali ya maendeleo ya kiuchumi, katika nchi hizi, na matokeo yake ni kiwango bora cha maisha kwa mamilioni ya watu na hatimae hawata endelea kuishi katika umasikini wa hali ya juu.

Benki ya dunia na IMF imeonya kuwa katika nchi nyingi zinazoendelea idadi ya watu masikini haitapungua sana. Haswa katika maeneo ya Afrika, kusini mwa Sahara. Kwa mujibu wa ripoti hii, kwenye maeneo haya kuna uwezekano umasikini ukaongezeka kwa asilimia 10, ifikapo mwaka 2015. Zia Qureshi wa Benki ya dunia na mwandishi mkuu wa ripoti hii, amesema kuna uwezekano eneo la Afrika, kusini mwa Sahara, lisiweze kutimiza malengo ya milenia kama sera za maendeleo katika nchi hizi hazitabadilishwa.

Qurashe amesema kuna umuhimu wa kuongeza misaada. Lakini pia nchi hizi zinatakiwa kuboresha sera zao na jinsi wanavyotumia misaada hiyo. Kuongeza misaada kunatanakiwa kuendana na mfumo mzima wa kuinua uchumi na kuongeza bidii ya kuwafikishia watu huduma muhimu. Suluhisho sio kuongeza tu misaada.

Ripoti hii lakini ina mazuri juu ya baadhi ya nchi za Kiafrika. Kwa kipindi cha miaka kumi nchi kumi na mbili zikiwemo Ghana, Mali, Msumbiji, tanzania na Uganda, zimeweza kukuza uchumi kila mwaka kwa asilimia 5.5. Lakini kutokana na makadirio ya Benki ya dunia na IMF, nchi za Afrika zinahitaji kukua kwa asilimia 7, ili kufikia malengo ya milenia.

Waandishi wa ripoti hii wana wasiwasi mkubwa juu ya swala la afya. Qureshi anasema malengo ya afya ndio yako hatarini kutotimizwa kabisa.

Qureshi amesema kila wiki watoto 200,000 chini ya miaka mitano wanakufa kutokana na magonjwa mbalimbali. Kila wiki wanawake 10,000 wanakufa wakati wakijifungua. Mwaka huu watu milioni mbili watakufa afrika, kusini mwa Sahara, kutokana na UKIMWI. Na zaidi ya watoto milioni 115 hawaendi shule. Ukiangalia kwa undani takwimu za malengo ya mileni sio namba tu, utaona ni watu wanaoathirika na ukosefu wa maendeleo ya kutimiza malengo haya, na matokeo yake ni makubwa na yanahuzumisha.

Swala linaloonekana kwa wazi kuwa ni gumu kutimiza ni kuzuia uambukizaji wa UKIMWI, lengo ni kulitimiza ifikapo mwaka 2015. Mwaka uliopita watu milioni 3.5 walikufa kutokana na UKIMWI, idadi hii ni kubwa kuliko miaka mingine na mara nne zaidi, ukilinganisha na mwaka 1990.

Pia haielekei kama tatizo hili litapata ufumbuzi hivi karibuni. Mwaka jana tu watu milioni 5 wameambukizwa. Kuna nchi kama Brazil, Senegal, Kambidoa au Thailand, ambazo zimeweza kufanikisha kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa UKIMWI. Benki ya dunia na IMF zimeshutumu kwamba nchi chache zinafuata mfano kama huu. China, India na Urusi, baadhi ya nchi zenye watu wengi duniani, zinalaumiwa kwa kutofanya vya kutosha kuzuia uambukizaji wa UKIMWI.

Kwa upande wa ugonjwa wa Malaria, imeonekana fedha zaidi zinahitajika kupambana na ugonjwa huu.

Ili kufikia malengo ya mailenia, Benki ya dunia na IMF wameshauri mpango utakaofuata hatua tano. Kwenye mpango huo wamezitaka nchi zinazoendelea kuboresha sekta za elimu na afya. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuongeza mara mbili misaada yao na pia kufungua masoko yao kwa ajili ya bidhaa za kilimo kutoka nchi masikini.

Qureshi amesema ujumbe muhimu katika ripoti hii ni kama jumuiya ya kimataifa haita chukua hatua za haraka za kuwezesha maendeleo, basi malengo ya mailenia yako hatarini kutotimizwa.