1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka ya Amnesty International

Oumilkher Hamidou24 Machi 2009

China inaongoza orodha ya nchi zinazotekeleza adhabu ya kifo,katika wakati ambapo Marekani inaanza kuipa kisogo adhabu hiyo

https://p.dw.com/p/HIVx
Kitambulisho cha Amnesty International dhidi ya kunyongwa watuPicha: AP/DW


Idadi ya waliouliwa baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo ulimwenguni imefikia watu 2390 mwaka jana.Idadi hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asili mia 90 ikilinganishwa na mwaka 2007.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika linalopigania haki za binaadam Amnesty International iliyochapishwa mjini London.


Katika ripoti hiyo ya mwaka,shirika hilo linalotetea haki za binaadam,lenye makao yake makuu mjini London,limekusanya maelezo kuhusu visa 2390 vya kuuliwa watu waliohukumiwa adhabu ya kifo katika nchi 25-ikimaanisha watu sabaa wameuliwa kwa siku mwaka jana.


Katika kipindi hicho hicho,watu  8864 wamehukumiwa adhabu ya kifo.Nchi tano; jamhuri ya watu wa China,Iran,Saud Arabia,Pakistan na Marekani zinabeba jukumu la kutekeleza asilimia 93 ya adhabu hizo za kifo.

Pekee jamhuri ya watu wa China imeamuru wahukumiwa 1718 wauliwe,ikiwa ni sawa na asili mia 72 ya kiwango jumla ulimwenguni.Hata hivyo Amnesty International inahisi idadi hiyo ni ya chini ,na ukweli wa mambo hasa haujulikani.


Barani Ulaya Byelorusia ni nchi pekee inayotekeleza adhabu hiyo baada ya kupigwa marufuku Uzbekistan.Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International jamhuri hiyo ya zamani ya usovieti imewauwa watu wanne mwaka jana.


Nchi Marekani watu 37 wameuliwa mwaka jana-18 kati yao wameuliwa katika jimbo la Texas.Hata hivyo idadi ya wanaouliwa imepungua sana tangu mwaka 1995 nchini Marekani.Amnesty International inahisi Marekani inaendelea kuipa kisogo adhabu ya kifo.Katika kampeni yake ya uchaguzi rais wa Marekani Barack Obama alisema hata hivyo:


"Nnahisi kuna sababu fulani zinazofanya kua adhabu ya kifo inafaa.Kuna uhalifu uliokidhiri,kwa mfano ugaidi au kuingiliwa kimwili watoto ambapo adhabu ya kifo inastahiki kutumika."


Thuluthi mbili ya mataifa ya dunia yameachana na adhabu ya kifo na kati ya nchi 59 ambako adhabu hiyo inatambuliwa kisheria,25 tuu ndizo zinazoitekeleza.


Eneo la mashariki ya kati na Afrika kaskazini zinakamata nafasi ya pili baada ya Asia ambako watu wengi wameuliwa mwaka jana.


Kwa mujibu wa Amnesty Internationa Iran imekwenda kinyume na sheria za kimataifa kwa kuwajumuisha watoto wanane kati ya watu 346 waliouuliwa kufuatia hukmu ya adhabu ya kifo.


Katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara watu wawili wameuliwa  Botswana na Sudan mnamo kipindi cha mwaka jana,ingawa 362 wamehukumiwa adhabu ya kifo barani humo mwaka jana.


"Habari za kutia moyo ni kwamba idadi ndogo tuu ya nchi ndizo zinazotekeleza adhabu ya kifo-hiyo ni ishara kwa mba tunaelekea katika ulimwengu usiokua na adhabu ya kifo." amesema hayo,katibu mkuu wa Amnesty International bibi Irene Khan .


MuandishiHamidou Oummilkheir/AFP/Reuters


Mhariri Abdul-Rahman Mohammed