Ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya Mauaji ya Bhutto.
16 Aprili 2010Matangazo
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo la watu watatu wakiongozwa na
Balozi wa Chile katika Umoja wa Mataifa Heraldo Munoz,
iliwasilishwa jana kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Ripoti imesema kwamba mauaji ya bibi Bhutto yangeweza kuzuilika
iwapo hatua za kutosha za kiusalama zingechukuliwa na kwamba
jopo hilo lililokuwa na kazi ya kuweka wazi jambo ambalo lilitendeka
na mazingira ya mauaji hayo, limesema linaamini kwamba kushindwa
kwa polisi wa Pakistan kuchunguza mauaji hayo ipasavyo kulikwa ni
kile walichokiita makusudi au kwa kudhamiria, kutokana na maafisa
hao wa polisi kwa kiasi fulani kuogopa kujihusisha kwa mashirika ya
kijasusi, katika uchunguzi huo.
Aidha ripoti hiyo pia imesema uchunguzi huo uliofanywa na tume
hiyo ya Umoja wa mataifa ulikuwa ukizuiwa vikali na mashirika ya
kipelelezi pamoja na maafisa wengine ambao walikuwa
wakikwamisha kutafutwa kwa ''ukweli ulio huru.''
Ripoti hiyo pia imeeleza kwamba Rais wa wakati huo Pervez
Musharaff alikuwa akitambua vitisho vinavyomkabili bibi Bhutto lakini
serikali yake hauchukua hatua zozote madhubuti, huku ikieleza
kubaguliwa kwa Bibi Bhutto tofauti na mawaziri wengine wakuu wastaafu ambao walikuwa wakipewa ulinzi mkubwa.
Benazir Bhutto, mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu nchini
Pakistan aliuawa Desemba 27, mwaka 2007, katika shambulio la
kujitoa mhanga, baada ya kuhutubia mkutano katika kampeni za
uchaguzi mjini Rawalpindi, mji ambao uko karibu na mji mkuu wa nchi
hiyo Islamabad.
Kifo chake hicho kilisababisha ghasia katika taifa hilo pekee la
kiislamu linalomiliki silaha za nyuklia, na kwamba ghasia hizo
zilimalizika baada ya mumwe bibi Bhutto Asif Ali Zardari kushinda
uchaguzi wa raia nchini humo.
Ripoti hiyo lakini haikumtaja mtu wanaeamini kuhusika na mauaji
hayo , lakini imependekeza kuwa uchunguzi wowote utakaostahili
kufanywa, lazima uangalie wale wote waliohusika kufikiria, kupanga
na kufadhili operesheni hiyo na pia wasiache kuondoa uwezekano
wa kuhusika kwa jeshi la pakistan.
Ripoti hiyo ilifanikishwa baada ya kuhoji watu zaidi ya 250, kukutana
na maafisa wa serikali, raia wa kawaida, raia wa kigeni wenye
kuyaelewa matukio hayo pamoja na wachunguzi wa kitengo cha
kupambana na ugaidi kutoka katika jeshi la polisi la Uingereza -Scotland Yard- ambao walisaidia kuchunguza mauaji hayo.
Hata hivyo kiongozi wa jopo hilo la uchunguzi la umoja wa mataifa
balozi Heraldo Munoz kutoka Chile amewaambia waandishi wa habari
kwamba , uchunguzi huo walioufanya, ulioanza Julai mwaka jana
haukuwa uchunguzi wa makosa ya jinai.
Wakati huo huo serikali ya Pakistan imesema itatoa kauli yake juu
ya ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo lililoteuliwa na Umoja wa Mataifa
baada ya kumaliza kuisoma.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp,Reuters)
Mhariri: Sekione Kitojo.
Matangazo