Maandamano kumkumbuka Brown yakumbwa na ghasia
10 Agosti 2015Maandamano hayo kumkumbuka Michael Brown aliyeuawa tarehe 9 August mwaka jana akiwa na umri wa miaka 18, yalikuwa yamefanyika kwa amani, yakiwashirikisha watu takribani 300, ambao walikaa kimya kwa dakika nne na nusu, na kupeperusha njiwa wawili weupe. Muda huo unawakilisha masaa manne na nusu ambayo maiti ya Brown ililala kifudifudi barabarani kabla ya kuondolewa.
Ghasia zilizuka baada ya kundi la watu wapatao 50 kuvamia duka la bidhaa za urembo katika kitongoji cha mji wa St. Louis na kuanza kufanya uporaji. Baadaye jioni maandamano hayo yalizidi kughubikwa na mvutano, ingawa hakukuwa na taarifa kuhusu yeyote aliyekamatwa.
Milio ya risasi ilianza kusikika pale polisi walipotaka kulitawanya kundi la waandamanaji lililokuwa likijaribu kuziba barabara na kuvunja madirisha ya nyumba katika mtaa ambao ulikuwa kitovu cha uhasama wakati wa maandamano ya mwaka jana, yaliyofuatia kuuawa kwa Michael Brown.
Polisi wasifiwa kwa 'mbinu sahihi'
Mkuu wa Polisi katika mji wa Ferguson Andre Anderson, amesema kwa sehemu kubwa maandamano yaliendeshwa kwa amani, na amesifu mbinu zilizotumiwa na polisi katika maandamano ya jana.
''Nadhani mkakati wa polisi ulikuwa bora zaidi mara hii. Sababu pekee ya kuweka polisi waliojihami, ni waandamanaji ambao wameanza kuwarushia chupa maafisa wetu wakidhamiria kuwadhuru''. Amesema afisa huyo.
Wengi wa wale walioshiriki katika maandamano ya Jumapili walivaa T-shirt zenye picha ya Michael Brown, na maandishi yasemayo, ''Choose Change'', maana yake, chagua mabadiliko. Wengine walikuwa na mabango yasemayo, ''Acha kuuwa watoto weusi''.
Baba mzazi wa Michael Brown amewashukuru walioitikia maandamano hayo, akisema isingekuwa uitikiajo wao huo, kila kitu kingesahaulika.
Mshikamano katika kumbukumbu
Mbali na Ferguson, maandamano mengine yamefanyika mjini New York. Watu walikusanyika katika uwanja wa 'Union Square' kuonyesha mshikamano na wenzao wa Ferguson, kutaka wimbi la mauaji dhidi ya watu kutoka jamii za wachache yakomeshwe.
Viongozi wa jumuiya ya wamarekani weusi wamesema wameshuhudia mabadiliko makubwa kimtazamo kuhusu suala la ubaguzi wa rangi nchini Marekani mwaka mmoja baada ya Brown kuuawa, na kushangaa lakini kwamba hakuna makubwa yanayofanywa na wabunge kutaka mabadiliko ndani ya mfumo wa polisi nchini humo.
Ijumaa iliyopita polisi ilimuuwa kijana mwanafunzi na mchezaji wa soka katika jimbo la Texas, alipokuwa akiingiza gari lake katika lango la duka la kuuza magari.
Mkuu wa Shirika la Watu wasio wazungu nchini Marekani - NAACP, Cornel William Brooks amesema wabunge 40 wamechukua hatua kadhaa za kutaka kuliwajibisha jeshi la polisi, lakini ni chache tu miongoni mwa hatua hizo ambazo zimetekelezwa.
Ametaka sheria ipitishwe kuwakataza polisi kuwaandama watu kwa misingi ya rangi ya ngozi yao, kuwalazimisha polisi kuvaa kamera, na kuitaka mamlaka ya polisi kuonyesha stahamala katika utendaji wao wa kazi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga