RPF ya Rwanda yaadhimisha miaka 25
20 Desemba 2012Rais Paul Kagame ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho anatarajiwa kuhutubia taifa katika uwanja wa Amahoro mjini Kigali ambapo maadhimisho hayo yanafanyika. Viongozi mbali mbali wako nchini Rwanda kuhudhuria sherehe za maadhimisho hayo.
Tayari Rais wa Uganda Yoweri Museveni anasemekana amewasili nchini humo jana jioni na kulakiwa na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo pamoja na maafisa wengine wa serikali na wanadiplomasia kutoka nchi hizo mbili.
Viongozi wengine wanaohudhuria maadhimisho haya ni kutoka Burundi, Ethiopia, Sudan kusini, Msumbiji, Eritrea, na Afrika Kusini.
Chama tawala cha RPF-Inkotanyi kilianzishwa mwaka wa 1987 na kuchukua madaraka baada ya kuuangusha utawala uliokuwepo wakati wa mauaji ya kimbari nchini humo mwaka wa 1994. Chama hiki kitakumbukwa kwa kusimamisha mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini Rwanda kabla ya kuanza kwa maadhimisho ya leo, Rais Kagame amesema chama cha RFP ni kama familia inayoangalia watu wake wote na kuzingatia matakwa yao na pia kuwapa haki sawa. Rais huyo wa Rwanda amesema chama hicho kinataka kuwa na maendeleo endelevu kwa nchi ya Rwanda.
Umoja wa Kitaifa
Uongozi wa chama cha RPF umeonyesha umoja kwa kuwa na mipango kadhaa ya upatanishi hasaa baada ya mauaji ya mwaka wa 1994 na kuwaleta Wanyarwanda pamoja kwa kufanya kazi pamoja na kuijenga nchi hiyo.
Kwa miaka mitano iliyopita chini ya utawala wa RFP zaidi ya Wanyarwanda milioni moja wamejiondoa kutoka katika umaskini, na nchi hiyo inaendelea vizuri katika kutimiza malengo yake ya maendeleo ya millennia. Kulingana na utafiti wa kitaifa wa kuhesabu watu nchini humo uliofanyika mwaka huu nchi hiyo ina takriban idadi ya watu milioni 10.5.
Lawama kwa RPF
Hata hivyo kando na sifa nyingi zinazomiminiwa chama tawala cha RFP, utawala huo pia umekuwa ukishutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuchangia katika ghasia zinazoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Rwanda inasemekana kuwapa usaidizi waasi wa M23 wanaopigana na serikali ya DRC.
Wakosoaji wa Rwanda pia, wanaushutumu uongozi wa chama cha RFP kuwa unakandamiza sana haki za binaadamu, ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari na hata kutovumilia upinzani wowote wa kisiasa.
Ndani ya miaka hii 25 ya uhai wake, viongozi na wanachama kadhaa waandamizi wa chama hicho wamejikuta wakiadhibiwa kwa namna mbalimbali huku wengine wakilazimika kuikimbia nchi yao na kuishi uhamishoni.
Mwandishi: Amina Abubakar/ The New Times
Mhariri: Saumu Yusuf