1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

RSF: Tuko tayari kusitisha mapigano Sudan

20 Aprili 2023

Kiongozi wa jeshi la wanamgambo RSF Sudan Jenerali Hamdani Dagalo amekiambia kituo cha Al-Jazeera yuko tayari kusitisha mapigano wakati wa sikukuu za Eid el-Fitri, baada ya siku kadhaa za mapigano na jeshi la serikali.

https://p.dw.com/p/4QMk9
Sudan Khartum | Kämpfe zwischen Armee und RSF-Miliz | General Mohamed Hamdan Dagalo
Picha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Hata hivyo, Dagalo amesema hayuko tayari kuzungumza na mkuu wa majeshi Abdel-Fattah al Burhan ambaye anamtaja kama "muhalifu". 

Wakati mkuu huyo wa RSF akisema hayo, taarifa ya jeshi ya muda mfupi uliopita ilisema wao pia hawana mpango wa kuzungumza na RSF ili kuumaliza mzozo huo na badala yake wanawataka kujisalimisha na kuongeza kuwa wako tayari kujadiliana nao kuhusu hilo. Wanasisitiza kwamba hakutakuwepo na jeshi jingine nje ya mfumo wa sasa wa kijeshi.

Wakaazi katika mji mkuu Khartoum wamesema kumeendelea kusikika milio ya risasi hii leo, wakati wengi miongoni mwao wakijaribu kuukimbia mji huo uliogubikwa na mapigano makali kati ya jeshi na wanamgambo RSF. Tagreed Abdin, ni miongoni mwao, aliyelalama kwamba hakuna mahala ya salama pa kukimbilia.

Ni hatua muhimu kwa ajili ya misaada

"Maisha hapa Kharoum hii leo naweza kusema bado ni magumu yaliyogubikwa na mashaka na uchovu. Watu hawana umeme na maji tangu Jumamosi mapigano yalipoanza. Jana Jumanne tulirudishiwa umeme hapa kwetu lakini wakati huohuo roketi liliangukia jirani na nyumba yetu, kwa hiyo ni kama hakuna mahali salama kwa sasa hapa Khartoum," alisema Abdin.

Sudan Khartum | Kämpfe zwischen Armee und RSF-Miliz
Moshi ukifuka Khartoum kufuatia mapiganoPicha: AFP

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO limezitolea mwito pande zinazozozana nchini Sudan kusitisha mapigano ili kuruhusu majeruhi kutibiwa pamoja na kufungua njia zitakazotumiwa na watoa huduma pamoja na magari ya kubebea wagonjwa.

Mkurugenzi wa dharura wa shirika hilo kikanda Richard Brennan amesema, hatua kama hiyo ni muhimu kwa ajili ya raia kupata chakula, maji na dawa na waliojeruhiwa kutibiwa na kuongeza kuwa kwa sasa ugumu wa mazingira unawazuia kufikisha huduma hizi, ingawa ameahidi kufanya hivyo mara hali itakapobadilika.

Katika hatua nyingine, ndege tatu zilizobeba wanajeshi 177 wa Misri kutoka Sudan zimewasili mjini Cairo, na kundi jingine la wanajeshi 27 wa kikosi cha anga wako chini ya uangalizi wa ubalozi wa Misri nchini Sudan. Jeshi la Misri limesema wanajeshi hao walikuwa mafunzoni nchini Sudan. RSF iliwazuia wanajeshi hao 27 baada ya kuvamia kambi yao ya Merowe kaskazini mwa Sudan siku ya Jumamosi.

Waziri wa Uingereza aaihirisha ziara yake Samoa

Kutoka N'djamena nchini Chad, mamlaka zimesema karibu wanajeshi 320 wa Sudan wamekimbilia nchini humo wakati mapigano yakiendelea nchini kwao. Waziri wa ulinzi wa Chad, Daoud Yaya Brahim amesema wanajeshi wengi walikimbilia Chad mapema wiki hii na wamenyang'anywa silaha.

Sudan Khartum | Kämpfe zwischen Armee und RSF-Miliz | General Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa jeshi Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: EL TAYEB SIDDIG/REUTERS

Amesema, wanawazuia wanajeshi hao, kwa kuwa rais wa Chad anataka kuepusha mtizamo kwamba amewaruhusu wanajeshi wa Sudan kufanyia shughuli zao kutokea nchini humo dhidi ya RSF. Mchambuzi wa masuala ya Afrika wa taasisi ya tathmini ya majanga ya Verisk Maplecroft Benjamin Hunger amesema Chad inajaribu kutoegemea upande wowote, ingawa kuna uwezakano inampinga Dagalo.

Na huko London, Uingereza, waziri wa mambo ya nje James Clevery ameahirisha ziara yake katika kisiwa cha Samoa, ili kuratibu jitihada za Uingereza katika kukabiliana na mzozo huo wa Sudan. Clevery ambaye kwa sasa yuko New Zealand alipangiwa kukutana na maafisa wa Samoa na waziri wa mambo ya nje Nanaia Mahuta, lakini badala yake alikwenda Wellington, New Zealand, baada ya mikutano katika ukanda wa Pasifiki.