1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RSF: Uhuru wa vyombo vya habari mashakani wakati wa COVID

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2021

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka RSF, inasema kwamba uhuru wa vyombo vya habari duniani kote umezuiliwa wakati wa janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3sH5v
Deutschland Symbolbild Pressefreiheit
Picha: Imago Images/S. Boness

Janga la ulimwengu la COVID-19 limechangia ongezeko la ukandamizaji na mashambulizi dhidi ya tasnia ya habari kote ulimwenguni, kulingana na ripoti iliyotolewa leo na shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka RSF.

Ripoti za habari zinazohusiana na maendeleo juu ya Covid-19 zimekuwa zikizuiliwa kwenye nchi nyingi kote ulimwenguni. Baadhi ya nchi zimeshuhudia serikali zake zikitumia mgogoro huo kuvibana vyombo vya habari, wakati nyingine ikiwemo Ujerumani kumekuwa na ongezeko la mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.

Mkurugenzi mtendaji wa RSF nchini Ujerumani Christian Mihr ameieleza DW kwamba "janga la virusi vya corona limezidisha tabia ya ukandamizaji kote ulimwenguni".

Lakini waandishi wa habari wamekuwa na jukumu muhimu sana katika kupambana na kuenea kwa habari za uongo zilizotolewa na viongozi kama vile rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, rais wa Brazil Jair Bolsonaro na rais wa Venezuela Nicolas Maduro.

Faharasi ya Uhuru wa vyombo vya habari mwaka 2021
Faharasi ya Uhuru wa vyombo vya habari mwaka 2021

Ingawa nchi za Ulaya zimechukua nafasi saba kati ya kumi zilizo orodheshwa na RSF katika Farahasi ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka wa 2021, ripoti hiyo inasema ni nchi tatu pekee za Norway, Finland na Sweden ambazo zilikuwa na uhuru wa vyombo vya habari uliolindwa vya kutosha.

Ripoti hiyo imeishutumu Uingereza kwa jinsi ilivyomshughulikia mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange ambapo imeporomoka kwa nafasi mbili ikiwa katika nafasi ya 33.

Ugiriki na Uhispania nazo zimemulikwa kwa kujaribu kuwazuia waandishi wa habari kuripoti juu ya wahamiaji pamoja na uamuzi wa kisiasa wa waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban wa kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari.

Ujerumani nayo pia imekosolewa kwenye ripoti hiyo kufuatia matukio mengi ya waandishi kushambuliwa wakati wa maandamano ya kupinga vizuizi vya corona na kuifanya kushuka nafasi mbili katika kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari hadi nafasi ya 13.

Maoni: Hali ngumu kwa vyombo vya habari Tanzania

Belarus ndiyo imekuwa na rekodi mbaya barani Ulaya, ambapo mwaka uliopita zaidi ya waandishi wa habari 400 walikamatwa na kushika nafasi ya 158 kati ya nchi 180. Nchi jirani ya Urusi ilijikongoja kidogo na kushika nafasi ya 150. Nchi za kiafrika kwa wastani zimeendelea kufanya vibaya huku Eritrea ikishika nafasi mbaya zaidi kote ulimwenguni. Afrika imeonekana kuwa hatari zaidi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo, baadhi ya nchi zimeonekana kuimarika. Burundi imepanda kwa nafasi 13 hadi nafasi ya 147 baada ya kuwaachia waandishi wa habari kadhaa waliokuwa wamefungwa kiholela.