1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Rumble in the Jungle" yakumbukwa baada ya miaka 50

30 Oktoba 2024

Oktoba 30 1974, Muhammad Ali alimpiga knockout George Foreman katika raundi ya nane ya pambano lililopangwa kuwa na raundi 15, maarufu kama "Rumble in the Jungle," lililofanyika Kinshasa, Kongo, na kurejesha taji lake.

https://p.dw.com/p/4mOPe
Muhammad Alis Meisterschaftsgürtel für 6,18 Millionen US-Dollar versteigert
Picha: AP/picture alliance

Alfred Mamba alikuwa na umri wa miaka 12 tu wakati bingwa wa ndondi Muhammad Ali alipowasili Kinshasa, mji mkuu wa Zaire wakati huo, mnamo Oktoba 1974 kwa nia ya kurejesha taji lake la uzito wa juu.

Mamba alitazama jinsi baba yake - ambaye alikuwa mwamuzi wa ndondi - alivyosaidia kubeba bendera kuingia uwanjani kabla ya pambano kati ya Ali na Mmarekani mwenzake George Foreman, lililofanyika majira ya alfajiri tarehe 30 Oktoba.

Kumbukumbu ya tukio hilo, maarufu zaidi kama "Rumble in the Jungle", imebaki kwake kwa miaka 50.  "Ilikuwa ni hali isiyoaminika, hatujawahi kuona mazingira kama hayo,” analiambia shirika la habari la AFP kwa bashasha, kandoni mwa Mashindano ya Ndondi ya Wanagenzi ya Afrika yaliyofanyika Kinshasa.

"Rumble in the Jungle", iliyomvutia Norman Mailer kuandika kitabu chake cha "The Fight" na kutengeneza filamu ya "When We Were Kings" iliyopewa tuzo ya Oscar, sasa ni hadithi ya kihistoria katika ndondi.

Mpambano huu ulifadhiliwa kama tukio la matangazo makubwa na dikteta wa Zaire, Mobutu Sese Seko, na kufanyika kwenye Uwanja wa 20 Mei, ambao sasa unajulikana kama Uwanja wa Tata Raphael, na ulioneshwa katika nchi zaidi ya 100.

Uwanja huo mkubwa wa zege uliingia watu takribani 60,000, wakiimba, kucheza, na kushangilia kwa hamu kabla ya mechi.

Muhammad Ali vs George Foreman 1974
Jasho likiruka kutoka kichwa cha Foreman anapopokea konde la mkono wa kulia kutoka kwa mpinzani wake Muhammad Ali katika raundi ya saba ya pambano la Rumble in the Jungle.Picha: AP

Mbinu ya Ali kuvutia mashabiki upande wake

"Watu walikuwa wakipiga kelele kila wakati, ilikuwa hali ya kushangaza sana,” Mamba anakumbuka kwa macho ya mshangao, huku akipitia picha za rangi nyeupe na nyeusi za tukio hilo la kihistoria lililobadili mwelekeo wa maisha ya Ali.

Foreman, mshindi wa medali ya dhahabu kwenye Olimpiki ya Mexico 1968, ndiye aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya ushindi — akiwa na umri wa miaka 25, alikuwa ameshinda mapambano yake 37 ya kwanza tangu kuanza ngumi za kulipwa.

Soma pia: Kinshasa yamkumbuka Muhammad Ali

Foreman alianza kwa nguvu, lakini Ali, mwenye umri wa miaka 32, alitumia mbinu zake maarufu za "rope-a-dope" na kubadilisha hali ya pambano, akimpiga Foreman kwa "hook" ya kushoto na ngumi ya moja kwa moja ya kulia iliyomwangusha kwenye ulingo katika raundi ya nane. Foreman alijaribu kusimama, lakini mwamuzi aliashiria mwisho wa pambano na ushindi wa knockout kwa Ali.

Ulikuwa ushindi kwa Ali, aliyerejesha taji lake lililochukuliwa mnamo 1967 baada ya kukataa kujiunga na jeshi kwa ajili ya Vita ya Vietnam, hali iliyomuweka kwenye zuio la miaka mitatu na nusu.

"Watu walimtakia sana Muhammad Ali ushindi,” anasema Mamba. Hakukuwa na sababu ya wazi kwa nini wenyeji walimpenda Ali zaidi, lakini, kwa mujibu wa "The Africa Report", Ali alijenga sababu.

Wakati Foreman alipowasili Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) akiwa na mbwa wake wawili aina ya "German Shepherd", mbegu iliyopendwa sana na wakoloni wa Ubelgiji, Ali alisema Foreman alikuwa Mbelgiji, na watu walimuunga mkono.

"Muhammad Ali alipopiga ngumi ya mwisho, kila mtu alipiga kelele,” anasema Mamba.

DR Kongo | Uwanja wa Tata Raphael
Uwanja wa Tata Raphael, lilikofanyika pambano la "Rumble in the Jungle."Picha: Junior Kannah/AFP/Getty Images

"Ali Alikuwa Mmoja Wetu"

Katika mji wa Kinshasa, kumbukumbu ya pambano la kihistoria la Muhammad Ali dhidi ya George Foreman mwaka 1974 bado ipo hai na inathaminiwa sana na wenyeji, waliomchukulia Ali kama ndugu yao.

"Ali alikuwa Mkongo," anasema Martin Diabintu, mwamuzi wa mashindano ya ngumi za ridhaa Kinshasa, akisisitiza jinsi roho ya Ali ilivyowagusa sana watu wa Kongo.

Mchezo huu ulipangwa awali kufanyika Septemba 25, lakini uliahirishwa baada ya Foreman kuumia wakati wa mazoezi, jambo lililoongeza hamu ya ulimwengu mzima, hasa katika jiji la Kinshasa.

Boniface Tshingala, mwamuzi mwenza wa Diabintu, anakumbuka umati mkubwa uliotanda kilomita kadhaa nje ya Uwanja wa Tata Raphael siku ya pambano. Saa kadhaa kabla ya pambano kuanza, mashabiki walikuwa tayari wamejaa kila upande wa uwanja, wakitamani kushuhudia historia ikiandikwa.

Ingawa uwanja huo umefanyiwa marekebisho, ukiwa mwenyeji wa michezo mikubwa kama Michezo ya Francophone ya mwaka 2023, kumbukumbu ya "Pambano la Karne" bado ipo hai.Kinshasa yamkumbuka Muhammad Ali

Diabintu, aliyekuwa bondia zamani, anatafakari juu ya urithi huu, akilitaja kuwa "pambano la karne" – jina ambalo limebakia kwa nusu karne sasa.

"Rumble in the Jungle": Miaka 50 ya Urathi wa Muhammad Ali

Ndoto Iliyotimia: Jinsi 'The Rumble in the Jungle' Ilivyochochea Kizazi cha mabondia wa Kongo

Sasa akiwa na umri wa miaka 64, Diabintu alikuwa kijana tu wakati Muhammad Ali na George Foreman walipofika Kinshasa. Alikuwa na hamu sana ya kushuhudia pambano hilo kiasi cha kutembea kilomita 10 kutoka nyumbani kwake hadi uwanjani.

"Nilikuja kwa miguu. Baada ya kumaliza shule, nilikuja kuangalia pambano," anasema. Tukio hili lilimvutia zaidi ya udadisi na lilibadilisha maisha yake, akianza kama bondia na hatimaye kuwa kocha na mwamuzi. "Ni tukio hili lililonisukuma kuingia kwenye masumbwi," anaeleza kwa shukrani.

Wote watatu, ambao walikuwa mabondia zamani, wanaeleza kwa fahari jinsi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilivyofanikiwa kuandaa tukio hili kubwa ambalo bado linaishi katika kumbukumbu hata baada ya miaka hamsini.

"Watu hawakuamini kwamba DRC ingeweza kuandaa pambano hili, lakini tulifanikiwa kwa asilimia 100," anasema Mamba kwa kujivunia.