Ruto amuomba msamaha Kenyatta
26 Mei 2022Kwenye hotuba yake ya mwisho kama naibu wa rais wa Kenya, kinyume na itifaki, William Ruto alimualika mgombea mwenza wa urais wa chama cha Azimio la Umoja One Kenya, Martha Karua kulihutubia taifa kama mwakilishi wa Raila Odinga anayewania urais .Martha Karua amesisitizia umuhimu wa kufanya kampeni pasina matusi na kauli chafu.
Bi Karua amesema,”sala bila vitendo sio kweli. Naomba sala zetu ziambatane na vitendo.Tukifanya hivyo tutakuwa na uchaguzi wa amani, mabadiliko ya serikali ya amani na taifa linalosimama pamoja.”
Kauli mbiu ya ibada ya kitaifa kwa mwaka huu ni mabadiliko au mapito inayoendana na uchaguzi mkuu ujao wa Agosti wakati serikali mpya itachukua hatamu. Kwa upande wake Naibu wa rais William Ruto aliwaomba waratibu radhi kwa kukiuka itifaki na pia kumtaka Martha Karua kutoa hotuba kwa kushtukizwa.
Kiongozi huyo wa UDA anayewania urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza alimuomba pia Rais Uhuru Kenyatta msamaha kwa kutotimiza baadhi ya matarajio kama naibu wake.Anasema anamuomba Mola awasamehe wote aliowakosea na waliomkosea ili waingie kwenye uchaguzi bila kinyongo.
Soma pia→Kenya kupata makamu wa Rais wa kwanza mwanamke?
Uhuru ahidi kuachia madaraka kwa mshindi wa uchaguzi
Kwa kawaida rais Uhuru Kenyatta hukaa meza moja na naibu wake ila kwa wakati huu William Ruto alikaa pamoja na spika wa bunge la taifa na yule wa baraza la Senate.Wawili hao ni wanachama wa muungano wa Kenya Kwana anaouwakilisha William Ruto. Wakati huohuo, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa pamoja na wawakilishi wa Idara ya mahakama Jaji Mkuu Martha Koome na Mwanasheria mkuu Paul Kihara.
Soma pia→Changamoto za kiusalama kuhusu uchaguzi Kenya
Kwenye hotuba yake ya mwisho kama rais katika ibada ya taifa, Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa wakati utakapofika atakikabidhi madaraka kikosi cha washindi wa uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu.
"Tunapojiandaa kwa uchaguzi ujao,tunajua kuwa ujenzi wa taifa ni wajibu wa kupokezana kutokea kizazi kimoja hadi chengine bila dosari nami natarajia kufanya vivyo hivyo.”
Ibada ya taifa ilifanyika kwenye hoteli ya kifahari ya Safari Park zikiwa zimesalia siku 74 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti.TM,DW Nairobi.