1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto kugombea urais wa Kenya kwa tiketi ya UDA

Admin.WagnerD15 Machi 2022

Wajumbe wa chama cha UDA wamemuidhinisha Naibu Rais William Ruto kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya, utakaofanyika tarehe tisa mwezi Agosti mwaka huu.

https://p.dw.com/p/48W3t
Kenia Präsident William Ruto
Naibu Rais wa Kenya William Ruto Picha: picture-alliance/Photoshot/P. Siwei

Ruto sasa atamenyamana na kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu. 

Ruto alipokewa na mkewe Rachel pamoja na maafisa wakuu wa chama cha UDA mwendo wa saa tano kasorobo katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani, uliokuwa na yamkini wajumbe 5000 waliokuwa na mavazi ya manjano na kijani.

Baadaye aliidhinishwa na wajumbe 4,350 wa UDA bila ya kupingwa kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwenye hafla iliyofanyika faraghani.

Kiunzi cha pili cha Ruto sasa baada ya kukabidhiwa jukumu la kuipeperusha bendera ya chama hicho, ni kumchagua makamu wake ikizingatiwa kuwa, jamii za mlima Kenya na Magharibi ya Kenya zinakimezea mate kiti hicho. Rigathe Gachagua na Musalia Mudavadi wa ANC wanapigiwa upatu wa kiti hicho.

Ruto asema Jubilee imepoteza mwelekeo 

Kenia amtierender Präsident Uhuru Kenyatta behält seinen Posten
Mahusiano kati ya Ruto na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya yamepwaya katika miaka ya karibuni Picha: Reuters/T. Mukoya

Akipokea ridhaa hiyo, Ruto aliutaja utawala wa chama cha Jubilee kama uliopoteza mwelekeo katika kipindi cha pili. Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga waliweka kando tofauti zao na kuanza kushirikiana, hali iliyomtenga Ruto katika masuala ya uongozi na kumlazimisha kuanzisha chama chake.

"Leo, ninajua bila ya shauku, ya kwamba wakati umefika wa kuwakilisha walala hoi. Wakati umewadia wa kufika mwisho wa safari na kuweka walala hoi kwenye meza ya maamuzi.” amesema Ruto

Naibu Rais ambaye amegeuka kuwa hasimu mkubwa ndani ya serikali anayohudumia, alikabiliwa na washindani wawili kwenye kiti hicho katika uteuzi chamani. Nancy Wanjiru mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu na Orina Japhanei.

Hata hivyo Nancy na Orina hawakufaulu baada ya kukosa fedha za kulipa kuwania. Walihitaji shilingi nusu milioni kama shuruti la chama.

Uchaguzi wa patashika nguo kuchanika

Uhuru Kenyatta Empfang in Kenia 9. Oktober
Picha: Reuters/Noor Khamis

Ruto alikosoa taasisi za serikali kwa kutumiwa kuwavuruga pamoja na washirika wake, hali ambayo alisema ataifuta iwapo atachaguliwa kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.

Mwenyekiti wa chama cha UDA Johnstone Muthama amesema "Sisi kwa umri ni mwaka mmoja na nusu, lakini kwa matendo na umaarufu tuna umri wa miaka 50. Sasa tuna kibarua cha kuhakikisha kuwa tunashinda na kuunda serikali.”

Huku akiwatetea wanyonge, Ruto aliutaja uchaguzi mkuu ujao kuwa utakaoshindaniwa kati ya walala heri dhidi walala hoi.

Aliwakosoa wapinzani wake, kwa kuwa na kiu ya uongozi ili kubadilisha katiba, na kugawana madaraka.

Mpango wa Maridhiano wa Kitaifa ulilenga kupanua nafasi za uongozi ili kuwakilisha makabila yaliyoko Kenya, hata hivyo bunge lilishindwa kupitisha mswada huo.

Kwa upande wake Ruto alielezea kuwa chama chake kikichaguliwa, kitajitahidi kuinua uchumi wa taifa kwa kubuni nafasi za kazi.

Zikiwa zimesalia siku 146 kwa uchaguzi mkuu kufanyika nchini Kenya, mwelekeo wa jinsi uchaguzi mkuu utakavyokuwa umeanza kudhihirika, huku homa ya uchaguzi ikiendelelea kusambaa kote.