1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruzuku za petroli na dizeli zasimamishwa Sudan

9 Juni 2021

Sudan imeondoa ruzuku katika bei za petroli na dizeli. Wizara ya fedha ya Sudan imesema bei za awali zitafutwa na bei mpya zitaanza kutumika zikiambatana na gharama za kuagiza.

https://p.dw.com/p/3udJv
Angola Tankstelle in Luanda
Picha: Getty Images/AFP/S. de Sakutin

Hatua hiyo ilipitishwa hapo jana ambapo sasa bei ya mafuta itaongezeka. Bei ya petroli itapanda kutoka pauni 150 za Sudan kwa lita moja hadi pauni 290, wakati bei ya dizeli iikifikia pauni 285 kwa lita tofauti na 125 za awali.

Wizara ya fedha imesema katika siku za usoni bei ya bidhaa hizo itaamuliwa kwa kuzingatia gharama za usafirishaji, ushuru, na kiwango cha faida.

Wizara ya fedha imesema ruzuku ya mafuta iliigharimu Sudan dola bilioni 1 kwa mwaka na iliwanufaisha watu wa matabaka ya kati na juu kuliko wenye kipato cha chini.

Hata hivyo, wizara ya fedha ya Sudan haikutangaza bei ya petroli inayozalishwa ndani ya nchi hiyo ambayo kwa kawaida gharama yake huwa ya chini.

Sudan imekuwa ikitekeleza mageuzi chini ya uangalizi wa shirika la fedha la kimataifa IMF kwa matumaini ya kuugeuza uchumi wake, kufikia lengo la kupata nafuu ya ulipaji wa madeni na kufanikisha uwezekano wa kupata ufadhili mpya.