Rwanda na Congo wakubaliana kusitisha uhasama
7 Julai 2022Taarifa ya ofisi hiyo ya rais wa Congo imesema kwenye mazungumzo hayo ya pande tatu, wakuu wa mataifa hayo Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Paul Kagame wa Rwanda na mwenyeji wa mazungumzo rais Joao Lorenco wa Angola wamekubaliana kusitisha uhasama mara moja na kulitaka kundi la wanamgambo wa M23 kujiondoa nchini Congo. Aidha mazungumzo yaliyozorota kuhusu mahusiano kati ya Rwanda na Congo yataanzishwa upya mjini Luanda Julai 12.
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ni kuhakikisha kwamba wanalikabili kundi la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda, FDLR. Kundi hilo la wanamgambo wa kabila ya Hutu linashutumiwa na Kigali kuendesha mapambano kwa kushirikiana na jeshi la Congo, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa ofisi ya rais wa Rwanda jana jioni.
Baada ya mkutano huo rais wa Rwanda Paul Kagame alisema anatarajia makubaliano hayo yatatekelezwa na mataifa hayo kurejea katika hali ya kawaida.
Amesema "Pia namshukuru rais Tshisekedi kwa michango yake inayotuwezesha nasi kuchangia ili mambo yasonge mbele na tunatarajia kurejesha mahusiano ya nchi zetu katika hali ya kawaida kwa kutatua pia masuala yanayoendelea huko kwetu ambayo yametufikisha hapa.
Rais Felix Tshisekedi amenukuliwa akisema anaamini mchakato huo utahitimisha haraka uhasama na mapigano na kurejesha utulivu kwenye mataifa hayo.
"Natumaini mchakato huu utasababisha mapigano kusitishwa mara moja na kundi la M23 kuondoka na ninatarajia utekelezaji wa mpango huo unaweza kutufikisha kwenye mchakato wa amani, utulivu na kuaminiana." alisema Tshisekedi.
Hali ya wasiwasi na mivutano ya kidiplomasi iliongezeka kwa kasi kati ya majirani hao wawili tangu kundi la wanamgambo wa M23 kuanzisha mashambulizi makubwa mashariki mwa Congo mwishoni mwa mwezi Machi. Congo imekuwa imishutumu Rwanda kwa kulisaidia kundi hilo. Hata hivyo Kigali inakana shutuma hizo na badala yake iliishambulia Congo kwa kulisaidia kundi la waasi ambalo wanamgambo wake wanadaiwa kushiriki mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, ingawa pia Congo inakana.
Tizama Picha:
Umoja wa Afrika mapema mwaka huu uliiomba Angola kuwa mpatanishi kati ya Rwanda na Congo chini ya mwamvuli wa chombo cha kikanda kinachojulikana kama Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Karibu watu 170,000 wameyakimbia makazi yao tangu M23 iliporejea mashariki mwa Congo, na kwenye mkutano huo wa kilele wa jana, wakuu hao walitoa mwito kwa wakimbizi wote kurejea kwenye mataifa yao, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya rais wa Congo.
Mashirika: RTRE