1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda na Uganda Matatani

MjahidA17 Oktoba 2012

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliotolewa hii leo inasema waziri wa ulinzi wa Rwanda aliamuru uasi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, unaofanywa na kundi la M23 linalopewa silaha na Rwanda na Uganda.

https://p.dw.com/p/16RIC
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Reuters

Ripoti hiyo inasema nchi hizo mbili Uganda na Rwanda zilituma wanajeshi nchini Congo  kwa waasi ili kulishambulia jeshi la kulinda amani la Umoja huo.

Kulingana na kundi la wataalamu kutoka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya Rwanda na Uganda kukana madai kuwa zinatoa usaidizi kwa kundi la waasi la M23, bado zinaendelea kutoa msaada mkubwa kwa waaasi hao  katika vita vyao vya miezi sita dhidi ya vikosi vya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo, kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini.

Ripoti hiyo ya kurasa 44 iliyoonekana mwanzo na shirika la habari la Reuters, inasema kuwa wakati maafisa wa Rwanda wakipanga muelekeo wa kundi hilo la M23 na pia kupanga jeshi lake kuungana na kundi hilo, Uganda ilikubali kundi hilo la waasi katika tawi lake la kisiasa kufanya kazi katika maeneo ya Kampala ili kujiimarisha zaidi.

Jeshi la DRC linalopambana na waasi wa M23
Jeshi la DRC linalopambana na waasi wa M23Picha: Reuters

Bosco Ntaganda, Kiongozi wa waasi DRC anayetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita  ICC  anaendesha uasi huo huku mkuu wa kundi la M23 Sultani Makenga akipanga namna kundi hilo litakavyofanya kazi na jeshi la Rwanda na Uganda.

Ntaganda na Makenga wanasemekana kupokea amri za kijeshi moja kwa moja kutoka kwa Jeshi la Rwanda, mnadhimu mkuu wa jeshi la Rwanda  Generali Charles Kayonga ambaye anapokea amri  kutoka kwa waziri wa ulinzi Generali James Kabarebe.

Rwanda na Uganda yakanusha madai

Awali Rwanda na Uganda ilikanusha madai kuwa inatoa usaidizi kwa kundi la waasi la M23. Msemaji wa jeshi nchini Uganda Felix Kulayigye ameyapuuza madai ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa huku akiwataka watoe ushahidi wa kutosha juu ya madai hayo. Kulayigye amesema baadhi ya wataalamu wa Umoja huo walifika nchini Uganda lakini hakuna mtu yeyote waliyemhoji kuhusiana na kisa hicho.

Wakaazi wa Kongo walioachwa bila makao
Wakaazi wa Kongo walioachwa bila makaoPicha: AP

Kwa upande wake Olivier Nduhungirehe, ambaye ni mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa pia amekanusha madai hayo. Amesema wataalamu wa Umoja huo wamepewa nafasi ya kuendesha suala hili kisiasa jambo ambalo haitasaidia kupata ukweli juu ya ghasia zinazoendelea katika Jamhuri ya kidemkorasia ya kongo.

Zaidi ya watu nusu milioni wameachwa bila makaazi kufuatia mapambano ya kundi hilo la waasi na vikosi vya serikali ya DRC. Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Mtaifa Herve Ladsous awali alisema kuwa kundi la M23 limeanzisha utawala wake Mashariki mwa Congo na kuanza kuwatoza ushuru wakaazi wa eneo hilo.

Mwandishi :Amina Abubakar/(Reuters)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman