SADC yatakiwa kukemea ukandamizaji nchini Zimbabwe
6 Agosti 2020Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limezitolea mwito nchi za Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, kukemea hadharani ukandamizaji uliofanywa na serikali ya Zimbabwe dhidi ya maandamano ya amani ya kupinga ufisadi yaliyofanyika Julai 31.
Shirika hilo pia limelaani kamata kamata ya kiholela dhidi ya wapinzani nchini humo.
Katika ripoti yake iliyochapishwa leo, Human Rights Watch inasema kuwa serikali ya Zimbabwe imewakamata kuhusiana na maandamanano hayo, watu wasiopungua 60, miongoni mwao akiwemo mwandishi wa vitabu Tsitsi Dangarembga na msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC Fadzayi Mahere.
Watu 16 walipatata majeraha yaliyowalazimu kutibiwa hospitalini, imeongeza ripoti hiyo. Dangarembga aliachiwa kwa dhamana siku moja baadaye.
Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika ukanda wa kusini mwa Afrika Dewa Mavhinga amesema SADC na Umoja wa Afrika, AU zinapaswa kuikemea serikali ya Zimbabwe kwa ukandamizaji huo na vitendo vingine vya uvunjifu wa haki za binadamu vinavyofanyika katika maeneo yote ya nchi, na kuueleza bayana uongozi wa rais Emmerson Mnangagwa kuwa vitendo hivyo vinakwenda kinyume na mikataba ya Umoja wa Afrika kuhusu haki za binadamu, na kwamba hilo halikubaliki.
Mkurugenzi huyo ameisifu Afrika Kusini kwa kujitokeza na kuelezea wasiwasi wake, akisema ingawa sio ncho zote za SADC zenye ujasiri wa kufanya hivyo, hilo pekee lina umuhimu wake.
''Inatia moyo kuona Afrika Kusini ikielezea wasiwasi wake, na kujihusisha na kampeni ya mtandani wa 'maisha ya Wazimbabwe yana thamani'. Hata kama hatuisikii kila nchi ya SADC ikiikemea hali nchini Zimbabwe, sauti ya Afrika Kusini kama taifa kubwa, inatosha.'' amesema Mavhinga.
Kuna visa vingi vya ukandamizaji
Ripoti hiyo ya Human Right Watch inaorodhesha visa vya kuwakamata kinyume cha sheria wakosoaji wa serikali nchini Zimbabwe, wakiwemo mwandishi wa habari aliyetuzwa kwa kazi yake Hopewell Chin'ono, na kiongozi wa kundi la kisiasa linalotaka mabadiliko la Transform Zimbabwe, Jacob Ngarivhume.
Chin'ono na Ngarivhume ambao wote wanasalia korokoroni kwa tuhuma za uchochezi, walisaidia kuanika kweupe ubadhirifu unaofanyika katika ngazi za juu serikalini, na kuhamasisha maandamano ya kitaifa ya Julai 31.
Mtu mwingine anayetajwa katika ripoti hiyo ni mwandishi wa habari maarufu Mduduzi Mathuthu, ambaye nyumba yake ilivamiwa na maafisa wa usalama Julai 30.
Baada ya kumkosa, ripoti hiyo inasema maafisa hao waliondoka na wapwa wake watatu pamoja na dada yake Nomagugu Mathathu, ili kumshinikiza mwandishi huyo kujisalimisha.
Mathathu anatuhumiwa pia kwa uchochezi na ghasia, kwa madai kwamba alikutwa na vipeperushi vyenye maandishi yanayosema ''Mnangagwa na baraza lake la mawaziri lazima wajiuzulu''. Baadaye aliachiwa na mahakama.
Orodha ni ndefu ya visa hivyo na wanaharakati waliojikuta uso kwa uso na mkono wa serikali.
Kufuatia ukandamizaji huo wa serikali ya Zimbabwe, kamishna wa Umoja wa Afrika anayehusika na haki za binadamu Solomon Dersso alisema kupitia mtandao wa twitter kwamba wanafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini Zimbabwe, na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuheshimu misingi ya haki za binadamu, hata wakati huu wa kupambana na janga la COVID-19.
Mwandishi: Daniel Gakuba/report
Mhariri: Iddi Ssessanga