1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yasaka suluhu Yemen Kusini

26 Agosti 2019

Muungano unaongozwa na Saudi Arabia, dhidi ya Wahouthi nchini Yemen umetoa wito wa kusitisha mapigano kusini mwa nchi hiyo katika vita vya kuwania madaraka vilivyosababisha mpasuko katika muungano huo wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/3OW4A
Saudi-Arabien Treffen König Salman bin Abdulaziz mit Scheich Mohammed bin Said Al Nahjan
Picha: Getty Images/AFP/M. Al-Hammadi

Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, madola mawili makuu katika muungano wa mataifa ya Kiislamu ya madhehebu ya Sunni wameunda kamati ya pamoja kusimamia usitishaji mapigano kati ya waasi wa kusini wanaotaka kujitenga, wanaoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Saudia katika mikoa ya Byan na Shabwa.

Naibu waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia, Khalid bin Salman, amesema kuwa wanashirikiana Umoja wa Famle za Kiarabu kuleta usalama na uthabiti katika maeneo ya Aden, Shabwa na Abyan pamoja na kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa makundi ya Al Qaida na Daesh, au Dola la Kiislamu.

Jemen Krieg STC-Kämpfer (Southern Transitional Council) in Aden
Wapiganaji wa vuguvugu la wanaotaka kujitenga kwa Yemen Kusini wakiwa kwenye kifaru walichokiteka kutoka vikosi vinavyomuunga mkono rais Hadi.Picha: Getty Images/AFP/N. Hasan

Mapema mwezi huu waasi wanaotaka kujitenga walichukuwa udhibiti wa mji wa bandari wa Aden, kusini mwa Yemen, ambao ndiyo makao makuu ya muda ya serikali ya rais Abd Rabbu Mansour Hadi, na wiki iliyopita wakatanua udhibiti wao hadi kufikia mji mkuu wa mkoa jirani wa Abyan. Wapiganaji wa kusini wamekabiliana na wanajeshi wa serikali katika mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Shabwa.

Pande zote mbili ni sehemu ya muungano unaoongozwa na Saudia Arabia na kuungw amkono na mataifa ya magharibi, ambao uliingilia nchini Yemen mwaka 2015 dhidi ya Wahouthi, walioifurusha serikali ya Rais Hadi katika mji mkuu wa sanaa.

Lakini Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, lilichukuwa udhibiti wa mji wa Aden baada ya kuutuhumu upande unaoshirikiana na Hadi kwa kushiriki katika shambulizi la Wahouthi dhidi ya vikosi vya kusini.

Utekelezaji wa makubaliano ya amani watatizwa

Vurugu hizo kusini mwa Yemen zimetatiza juhudi za Umoja Mataifa kutekeleza makubaliano ya amani kwingineko katika taifa hilola Kiarabu, na kusafisha njia ya majadiliano ya kumaliza vita vilivyouwa maelfu ya watu na kuisukuma Yemen kwenye kingo za baa la njaa.

Iran Jemen
Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Khamenei akikutana na msemaji wa vuguvugu la Wahouthi mjini Tehran.Picha: twitter/khamenei_ir

Taarifa ya Saudi Arabia imezisihi pande zote kushirikiana na kamati ya pamoja kuacha mapigano na kurudi kwenye maeneo yao, na imesisitza wito wa Saudi Arabi wa kufanyika mkutano wa kilele katika Falme hiyo ili kutatua mkwamo huo.

Serikali ya Mansour Hadi imesema haitoshiriki katika mazungumzo yoyote mpaka waasi wanaotaka kujitenga watakapo rudisha mamlaka ya maeneo walioyateka.

Wakati huo huo baraza la mpito la kusini  STC limesema halitokabidhi udhibiti wa kambi za kijeshi mjini Aden na maeneo mengine hadi chama cha Kiislamu cha Islah, ambacho ndiyo nguzo ya serikali ya Hadi, pamoja na watu kutoka kaskazini waondolewe kwenye nafasi za madaraka kusini.

Waasi wa Kihouthi ambao hivi karibuni wameongeza mashambulizi ya makombora na ndege zisizotumia rubani dhidi ya miji nchini Saudi Arabia, wanainyooshea kidolea Aden kama ushahidi kwamba Hadi, anaeishi mjini Riyadh, hafai kuongoza.

Chanzo: Reuters.