Scholz alaani shambulio lililowauwa watu watatu Solingen
24 Agosti 2024Shambulio hilo lilifanywa na mtu aliyejipenyeza kwenye tamasha la kusherehekea miaka 650 tangu kuanzishwa kwa mji huo lililohudhuriwa na maelfu ya watu Ijumaa usiku.
Kwa mujibu wa polisi wa mji huo, watu wanane walijeruhiwa na watano kati yao wanaripotiwa kuwa wamejeruhiwa vibaya. Akizungumzia mkasa huo Kansela Scholz amesema kuwa tukio la aina hiyo halikubaliki katika jamii na kwamba hatua kali za kisheria zinapaswa kuchukuliwa.
Soma zaidi: Waziri wa ulinzi wa Ujerumani alaani shambulio la kisu Solingen
Amelielezea shambulio hilo kuwa ni uhalifu wa kutisha na kwamba serikali itausaidia mji huo na watu wake kwa kila namna. Scholz ametoa pole kwa waliojeruhiwa na kutuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa waliouwawa katika shambulio hilo.
Kwa upande wake Rais wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier mapema Jumamosi alizungumza na meya wa Solingen, Tim Kurzbach.
Awali, Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser alisema kuwa, taifa hilo limeshtushwa na shambulio hilo la kisu la mjini Solingen. Feaser aliyetoa kauli yake kupitia jukwaa la X amelitaja shambulio hilo kuwa ni la kikatili na kuongeza kuwa, polisi wanafanya kila wawezalo ili kumkamata aliyehusika na shambulio hilo.
Msako mkali unaendelea
Taarifa ya polisi imesema kuwa kwa sasa msako mkali unaendelea ili kumpata mhusika wakati wakiendelea kuwahoji waathiriwa na mashuhuda wa tukio hilo. Polisi nchini humo imeanzisha pia ukurasa maalumu mtandaoni utakaowawezesha walioshuhudia kutoa taarifa zinazohusiana na tukio hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa watu waliohudhuria tamasha la Solingen waliripoti juu ya shambulio hilo majira ya saa tatu na nusu usiku, baada ya mshambuliaji kuwajeruhi watu watatu. Polisi wanasema mshambuliaji huyo ambaye bado hajajulikana alikimbia na uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtu huyo alipanga na kufanya shambulio hilo mwenyewe.
Tamasha hilo lililoanza Ijumaa lilipangwa kuendelea hadi Jumapili likisindikizwa na burudani ya muziki, kabareti na sarakasi. Hata hivyo shamra shamra hizo zilifutwa kabisa baada ya mkasa huo.
Vyanzo: Dpa/Reuters